Aug 15, 2016 03:43 UTC
  • Mamluki wa kundi lenye silaha watiwa mbaroni CAR

Askari jeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa waliopo Jamhuri ya Afrika ya Kati wametangaza kutiwa mbaroni mamluki kadhaa wa kundi moja lenye silaha nchini humo.

Wanajeshi hao wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wameeleza kuwa Jumamosi iliyopita waliwashambulia watu kadhaa waliokuwa na silaha waliokuwa katika magari saba kusini mwa mji wa Sibut nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati na kuwatia nguvu kumi kati yao. Wamesema kuwa watu wengine 25 kutoka kundi hilo walifanikiwa kukimbia. 

Maafisa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wamesema kuwa watu hao waliokamatwa ni wanachama wa kundi la waasi wa zamani wa Muungano wa Seleka.

Wanachama wa zamani wa Muungano wa Seleka

Wanachama wa kundi hilo tarehe 12 mwezi huu waliondoka Bangui mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati  ambapo wakiwa njiani waliwafyatulia risasi askari usalama katika vituo kadhaa vya upekuzi nchini humo.

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa waliopo Jamhuri ya Afrika ya Kati wamesema kuwa watu kadhaa waliuawa na wengine kujeruhiwa katika ufyatuaji huo wa risasi wa waasi wa zamani wa Seleka. Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika mapigano ya ndani mwezi Disemba mwaka 2012 na kusababisha ukosefu wa amani nchini humo na kupinduliwa serikali ya nchi hiyo. Raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati hivi sasa wana matarajio haya kuwa amani na uthabiti utarejea nchini kufuatia kuchaguliwa serikali na bunge jipya.

 

 

Tags