Kiongozi wa mapinduzi ya Guinea, Mamady Doumbouya aidhinishwa kuwania urais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133032-kiongozi_wa_mapinduzi_ya_guinea_mamady_doumbouya_aidhinishwa_kuwania_urais
Kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi wa Guinea Conakry, Mamady Doumbouya na wagombea wengine wanane wameidhinishwa kugombea katika uchaguzi wa rais mwezi ujao. Hii ni kwa mujibu wa orodha ya wagombea wa kiti cha urais iliyotolewa na Mahakama Kuu ya nchi hiyo.
(last modified 2025-11-11T03:05:44+00:00 )
Nov 11, 2025 03:05 UTC
  • Kiongozi wa mapinduzi ya Guinea, Mamady Doumbouya aidhinishwa kuwania urais

Kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi wa Guinea Conakry, Mamady Doumbouya na wagombea wengine wanane wameidhinishwa kugombea katika uchaguzi wa rais mwezi ujao. Hii ni kwa mujibu wa orodha ya wagombea wa kiti cha urais iliyotolewa na Mahakama Kuu ya nchi hiyo.

Doumbouya aliahidi kuwa hatogombea kiti cha urais alipotwaa madaraka ya nchi hiyo ya  Magharibi mwa Afrika mwaka 2021. Lakini katiba mpya iliyoshinikizwa na serikali inayoongozwa na jeshi na kuidhinishwa katika kura ya maoni mwezi Septemba, ilifungua mlango wa kugombea kwake.

Wakati huo huo imeelezwa kuwa wapinzani wawili wenye ushawishi, yaani Rais wa zamani wa Guinea Conakry Alpha Conde na Waziri Mkuu wa zamani Cellou Dalein Diallo, wamekosa sifa za kuwa wagombea kwa sababu ya sheria za umri na ukaazi kwa mujibu wa katiba mpya ya nchi hiyo. 

Mamady Doumbouya atachuana na wagombea wenye ushawishi mdogo kama vile Abdoulaye Yero Balde, waziri wa zamani wa elimu ya juu na naibu Gavana wa Benki Kuu, na Faya Millimono, kiongozi wa upinzani mkosoaji wa serikali.

Wakati huo huo chama cha Lansana Kouyate waziri mkuu wa zamani wa Guinea Conakry ambaye hajakubaliwa kugombea kiti cha urais kimesema kuwa kina mpango wa kukata rufaa. 

Serikali ya Doumbouya mwaka 2022 ilipendekeza kipindi cha uongozi wa mpito wa miaka miwili  baada ya kufanya mazungumzo na jumuiya ya kikanda ya ECOWAS, lakini ilishindwa kutimiza ahadi hiyo.

Uchaguzi wa rais wa Guinea Conakry uliopangwa kufanyika Desemba 28 unatazamiwa kuhitimisha rasmi kipindi cha serikali ya kijeshi kuelekea utawala wa kiraia.