Mkurugenzi Mkuu wa WHO ataka kusitishwa umwagaji damu nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133034-mkurugenzi_mkuu_wa_who_ataka_kusitishwa_umwagaji_damu_nchini_sudan
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ametaka kusitishwa ghasia nchini Sudan baada ya kuuawa daktari katika mji ulioathiriwa na vita wa Al Fasher.
(last modified 2025-11-11T03:09:52+00:00 )
Nov 11, 2025 03:09 UTC
  • Tedros Adhanom
    Tedros Adhanom

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ametaka kusitishwa ghasia nchini Sudan baada ya kuuawa daktari katika mji ulioathiriwa na vita wa Al Fasher.

"Umwagaji damu nchini Sudan ni lazima ukomeshwa," ameandika Tedros Adhanom katika mtandao wa kijamii wa X.

Amesema, amehuzunishwa na taarifa ya kuuawa Dkt Adam Ibrahim Ismail katika mkasa mwingine kwenye mji wa Al Fasher huko Sudan. Amesema Shirika la Afya Duniani  linaomboleza kifo cha Dkt Ismail na linatoa wito wa kukomeshwa ukatili dhidi ya wafanyakazi wa sekta ya afya.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO amemalizia ujumbe wake huo kwa kutoa wito wa amani akisema: "Amani ni dawa bora."

Tarehe 26 mwezi Oktoba mwaka huu wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) waliudhibiti mji wa Al Fasher na kufanya mauaji ya halaiki ya kikabila. Ripoti hii ni kwa mujibu wa mashirika ya ndani na ya kimataifa.

Mapigano yaliyoanza Aprili 2023 kati ya Jeshi la Sudan na kikosi cha RSF yameibua vita vya ndani nchini humo vilivyouwa maelfu ya wananchi wa Sudan na kupelekea mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. 

Wakati huo huo Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetoa mwito wa dharura wa kusaidiwa kimataifa maelfu ya watu waliokimbilia Chad kukwepa mauaji ya kimbari nchini Sudan. Wasudani wanaendelea kumiminika katika nchi jirani ya Chad kutoka eneo la Darfur la magharibi mwa Sudan.

Naibu Kamishna Mkuu wa UNHCR, Kelly Clements ametoa mwito huo baada ya kuwatembelea wakimbizi huko Farchana, Chad, ambao wamekimbilia nchini humo kutokea mji wa el-Fasher wa magharibi mwa Sudan.