WFP yaamua kupunguza mgao wa chakula kwa wanaokabiliwa na njaa nchini Sudan
-
WFP yapungua mgao wa chakula kwa wakimbizi, Sudan
Shirika la Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (WFP) limetangaza kwamba litaanza kupunguza mgao wa chakula unaotolewa kwa watu wa Sudan wanaokabiliwa na hatari ya njaa, kutokana na ukosefu wa ufadhili.
Ross Smith, mkurugenzi wa kitengo cha maandalizi na mwitikio wa dharura cha programu hiyo, amewaambia waandishi wa habari kwa njia ya video kwamba kuanzia Januari, taasisi hiyo "italazimika, kupunguza mgao wa chakula kwa 70% kwa jamii zinazokabiliwa na njaa, na kwa 50% kwa jamii zilizo katika hatari ya kutumbukia kwenye njaa."
Smith ametahadharisha kuhusu athari mbaya za ukosefu wa ufadhili wa shughuli za shirika hilo la misaada ya chakula nchini Sudan.
Ameongeza kuwa mgogoro wa ufadhili unaweza kuwa mbaya zaidi katika miezi ijayo, akieleza kuwa "kuanzia Aprili, tutakabiliwa na kuporomoka kwa ufadhili," jambo ambalo linatishia uwezo wa WFP kuendelea kukidhi mahitaji ya msingi ya chakula ya mamilioni ya watu nchini Sudan.
Mamilioni ya raia nchini Sudan wanakabiliwa na ugumu unaoongezeka wa kupata chakula cha kutosha, huku mgogoro unaosababishwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ukiendelea kuathiri miji, vijiji na kambi za wakimbizi.
Sudan imekuwa katika vita vya ndani kati ya jeshi la taifa na kundi la RSF tangu Aprili 2023, ambavyo hadi ssa vimesababisha mauaji ya makumi ya maelfu ya watu na kulazimisha wenghine milioni 13 kuhama makazi yao.