Maandamano dhidi ya Ufaransa yaongezeka nchini Burundi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13504-maandamano_dhidi_ya_ufaransa_yaongezeka_nchini_burundi
Maandamano ya kuipinga Ufaransa yanaripotiwa kuongezeka nchini Burundi.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Aug 18, 2016 03:13 UTC
  • Maandamano dhidi ya Ufaransa yaongezeka nchini Burundi

Maandamano ya kuipinga Ufaransa yanaripotiwa kuongezeka nchini Burundi.

Ripoti kutoka nchini Burundi zinasema kuwa, maandamano ya kupinga kupasishwa azimio nambari 2303 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopendekezwa na Ufaransa yanaonekana kuongezeka nchini humo. Waandamanaji hao wamekuwa wakiilaani Ufaransa na kupinga kutumwa nchibni humo polisi hao waangalizi.

Azimio hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linataka kutumwa nchini Burundi polisi waangalizi 228. Polisi hao wa Umoja wa Mataifa watakuwa na jukumu la kulinda usalama sambamba na kusimamia haki za binaadamu kwa ushirikiano na waangalizi wa kimataifa na wataalamu wa masuala ya kijeshi wa Umoja wa Afrika nchini humo. 

Machafuko ya Burundi

Philippe Nzobonariba, msemaji wa rais Pierre Nkurunziza ametangaza kuwa, kutumwa kwa polisi hao waangalizi kunakinzana na sheria za kimataifa na ni kukiuka mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo.

Itakumbwa kuwa, Burundi ilitumbukia kwenye mgogoro wa kisiasa kufuatia hatua ya chama tawala CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kugombea muhula wa tatu katika uchaguzi uliopita, machafuko ambayo hadi sasa yamesababisha mauaji ya watu zaidi ya 500 huku wengine zaidi ya laki 2 na 70 elfu wakilazimika kuitoroka nchi na kuwa wakimbizi.

Mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakikosoa kile yanachosema kuwa, ukiukaji wa haki za binadamu nchini Burundi.