Magaidi wanne wa ash-Shabab waangamizwa Somalia
Askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) wametangaza habari ya kuuawa wanachama wanne wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al Shabab nchini humo.
Joe Kibet, msemaji wa askari wa AU nchini Somalia amesema kuwa, magaidi hao wameangamizwa katika operesheni ya pamoja iliyoshirikisha askari wa serikali katika eneo la Bola-Galguduud, kusini mwa nchi hiyo. Ameongeza kuwa, hii ni operesheni ya pili iliyofanikiwa dhidi ya wanachama wa genge la sh-Shabab katika eneo hilo.
Kikosi cha askari wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) na askari wa serikali wameainzisha mkakati mpya kwa ajili ya kupambana na kundi hilo. Siku chache zilizopita pia askari hao walitangaza habari ya kuuawa wanachama watatu wa ash-Shabab katika eneo la kusini magharibi mwa mji wa Kismayo, huko kusini mwa mji wa Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.
Wakati huo huo, Umoja wa Afrika umetangaza kuwa, operesheni ya kuondoka askari wake nchini Somalia itaanza mwaka 2018, baada ya kuiwezesha serikali ya nchi hiyo kujidhaminia usalama wake yenyewe.