Shambulio la mabomu laua watu wasiopungua 20 Somalia
Watu wasiopungua 20 wameuawa katika miripuko miwili ya mabomu yaliyotegwa garini iliyotokea katika mji wa Galkayo ulioko kwenye makao makuu ya eneo linalojiendeshea mambo yake la Puntland nchini Somalia.
Kundi la kigaidi la Al-Shabab limetangaza kuhusika na shambulio hilo la leo la miripuko miwili ya mabomu iliyofuatana, ambalo lilitekelezwa na watu wawili waliojitolea mhanga waliokuwa wakiendesha magari hayo.
Ali Ahmed, Afisa wa Polisi wa mji wa Galkayo amethibitisha vifo vya watu hao wakiwemo raia na askari wa vikosi vya usalama.
Mashuhuda na wakaazi wa mji huo wamesema walisikia milio miwili mikubwa ya miripuko iliyofuatana, na kufuatiwa na milio mizito ya ufyatuaji risasi.
Halima Ismali, mkaazi wa mji wa Galkayo amevieleza vyombo vya habari kuwa mripuko wa kwanza ulikuwa wa bomu lililotegwa kwenye lori uliofuatiwa baada ya dakika moja hivi na mwengine wa bomu lililotegwa kwenye gari ndogo. Ameongeza kuwa kaka yake alijeruhiwa katika tukio hilo.
Duru za habari zinaeleza kuwa shambulio la kwanza lililenga makao makuu ya serikali katika mji wa Galkayo na lile la pili lililenga watu waliokuwa wakitoa huduma za dharura katika eneo la tukio la kwanza.
Ahmed Sugulem, daktari katika hospitali ya Galkayo amesema watu wengine 30 wamejeruhiwa katika shambulio hilo na idadi ya vifo inaweza kuongezeka.
Akithibitisha kuhusika na shambulio hilo la kigaidi, msemaji wa operesheni za kijeshi za Al-Shabab Abdiasis Abu Musab amesema kundi hilo limetekeleza mashambulio mawili ya kujitolea mhanga kwa kutumia magari mawili yaliyotegwa mabomu.
Kwa miaka kadhaa sasa vikosi vya serikali ya Somalia vikisaidiwa na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika vilivyotumwa nchini humo (AMISOM) vimekuwa vikipambana na kundi hilo lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda.
Vikosi hivyo vya pamoja vimefanikiwa kulifurusha kundi hilo la kitakfiri katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na katika miji mingine mikubwa ya nchi hiyo, lakini wanamgambo wake wanaendelea kufanya mashambulio ya hapa na pale katika sehemu mbalimbali za nchi.../