Chama tawala nchini Burundi chamteua Ndayishimiye kuwa mkuu mpya
Wajumbe wa chama tawala 'CNDD-FDD' nchini Burundi wamemchagua kwa wingi wa kura Meja Jenerali Evariste Ndayishimiye kuwa mkuu mpya wa chama hicho.
Kikao hicho ambacho kilihudhuriwa na Rais Pierre Nkurunziza, kimemchagua Ndayishimiye kuwa kiongozi mkuu wa chama hicho. Aidha katika kikao hicho ambacho kilifanyika mjini Gitega, mbali na kumchagua kiongozi mkuu wa chama, kimemchagua pia naibu na katibu mtendaji wa chama hicho.
Kabla ya kuchaguliwa katika wadhifa huo, Evariste Ndayishimiye alikuwa mshauri maalumu wa Rais Nkurunziza katika masuala ya mipango miji. Inafaa kukumbusha kwamba, Burundi ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa mwezi Aprili mwaka jana, kufuatia upinzani kwa hatua ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza azma yake ya kuwania urais kwa muhula wa tatu kwenye uchaguzi uliopita.
Kufuatia hali hiyo, kulijiri machafuko nchini humo ambayo yalipelekea mamia ya watu kuuawa na maelfu ya wengine kuwa wakimbizi. Kabla ya hapo pia Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alifanya safari nchini humo kwa lengo la kufanya mazungumzo na pande husika ili kuhitimisha hali ya mchafukoge nchini.