Rais wa Zambia ataka wapinzani waache fujo
-
Rais mteule wa Zambia, Edgar Lungu
Rais mteule wa Zambia, Edgar Lungu amewataka wapinzani wa nchi hiyo waache vitendo vya fujo na watumie njia za amani kuelezea malalamiko yao.
Gazeti la Lusaka Times limemnukuu Davies Chama, Katibu Mkuu wa chama tawala nchini Zambia cha Patriotic Front (PF) akisema kuwa, Rais mteule Edgar Lungu ametoa mwito kwa wapinzani waache mara moja machafuko na waoneshe malalamiko yao kwa njia za kisiasa na za amani.
Aidha amesema, rais mteule wa Zambia hana nia ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na mkuu wa chama cha upinzani cha UPND, Hakainde Hichilema.
Matamshi hayo ya chama tawala nchini Zambia yamekuja katika hali ambayo mamia ya wafuasi wa chama cha upinzani cha UPND wamewashambulia wafuasi wa chama tawala katika eneo la Namwala, kusini mwa Zambia na kupelekea raia 250 wa wilaya hiyo kukimbia makazi yao.
Huko nyuma pia, wafuasi wa chama cha UPND walivamia majengo ya taasisi za serikali ikiwa ni kulalamikia udanganyifu na kuchakachuliwa matokeo ya uchaguzi uliopita.
Tume ya Uchaguzi wa Zambia imetangaza kuwa, Edgar Lungu ameshinda uchaguzi huo uliofanyika tarehe 11 mwezi huu wa Agosti.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na tume hiyo, Edgar Lungu alipata kura karibu milioni moja na laki tisa na hivyo kumshinda mpinzani wake wa karibu, Hakainde Hichilema kwenye uchaguzi huo.