Ash-Shabab yashambulia tena mjini Mogadishu, watu kadhaa wauawa
Kundi la kigaidi na kitakfiri la ash-Shabab nchini Somalia limefanya shambulizi lingine mjini Mogadishu, mji mkuu wa nchi hiyo.
Duru za polisi nchini Somalia zimeripoti kwamba, jana jioni wanachama wa genge hilo walilipua bomu wakati wafanyakazi wa zimamoto kwa kushirikiana na polisi walipokuwa wakizima moto katika eneo la biashara la Suka-Holala, mjini Mogadishu, mji mkuu wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa polisi hiyo, raia wawili walipoteza maisha katika hujuma hiyo. Aidha polisi imeanzisha uchunguzi juu ya chanzo cha moto huo na kadhalika shambulizi hilo.
Hii ni katika hali ambayo Alkhamis usiku wanachama wa ash-Shabab walishambulia hoteli moja katika pwani ya mji wa Mogadishu na kusababisha watu 10 kuuawa. Wanachama wa genge hilo wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara nchini Somalia hususan mjini Mogadishu kwa lengo la kupambana na serikali ya nchi hiyo.
Hujuma za wanachama wa genge hilo maarufu kwa kutenda jinai zimeshadidi katika hali ambayo uchaguzi wa rais nchini humo umepangwa kufanyika hapo tarehe 30 Oktoba, huku ule wa bunge ukipangwa kufanyika tarehe 24 Septemba hadi 10 Oktoba mwaka huu.