Kuanza uchaguzi wa rais nchini Gabon
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i14071-kuanza_uchaguzi_wa_rais_nchini_gabon
Watu laki sita na elfu ishirini na nane waliotimiza masharti ya kupiga kura leo Jumamosi wameelekea kwenye masanduku ya kupigia kura huko Gabon kwa ajili ya kumchagua rais mpya wa nchi hiyo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Aug 27, 2016 09:20 UTC
  • Kuanza uchaguzi wa rais nchini Gabon

Watu laki sita na elfu ishirini na nane waliotimiza masharti ya kupiga kura leo Jumamosi wameelekea kwenye masanduku ya kupigia kura huko Gabon kwa ajili ya kumchagua rais mpya wa nchi hiyo.

Rais Ali Bongo Ondimba wa Gabon na Jean Ping Mkuu wa zamani wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ni washindani wakuu katika uchaguzi wa leo. Uchaguzi wa rais umeanza huko Gabon katika hali ambayo mivutano ya kisiasa imepamba moto  nchini humo kwa muda sasa kati ya wagombea wa kiti cha urais. Rais wa sasa wa Gabon ambaye anagombea tena katika uchaguzi wa leo,  alisema juzi katika mahojiano na kanali ya televisheni ya France 24 kuwa, yeye ni chaguo bora la kuleta mabadiliko huko Gabon.

 

Raia wa Gabon akitafuta  jina lake katika orodha ya wapiga kura

Ali Bongo ameashiria kushikilia hatamu za uongozi familia yake kwa muda wa karibu miaka 50 na kudai kuwa amekulia ndani ya utawala huo na anaufahamu vyema; na kwa msingi huo, yeye ni chaguo  linalofaa kwa ajili ya kuleta mabadiliko huko Gabon. Bongo ameongeza kuwa, alikuwa na mazungumzo ya wazi na baba yake ili kufahamu ni maeneo gani yanafanya vyema ili aweze kubeba jukumu la kuleta mabadiliko nchini kwa sababu fikra na mitazamo aliyonayo haina uhusiano wowote na yale yaliyojiri katika miaka ya karibuni.

Kuhusu swali lililohusiana na utambulisho wake pia, Rais wa Gabon alijibu kwa kusema wapinzani hawana sera wala ubunifu na kwamba wamefeli kikamilifu kwa upande wa sera. Amesema wapinzani wa Gabon hawana kazi ghairi ya kuzungumzia asilia yake katika hali ambayo walipasa kuwasilisha mipango wanayotaka kuwafanyia wananchi  wa Gabon badala ya kumzungumzia yeye.

Rais wa sasa wa Gabon Ali Bongo Ondimba anayegombea kiti cha urais

Wapinzani nchini Gabon wanasema kuwa Ali Bongo Ondimba amezaliwa nchini Nigeria na kwamba  anasema uwongo kuhusu mahali alipozaliwa. Wapinzani hao wanasema kuwa Ali Bongo hapasi kuwa rais kutokana na nchi alikozaliwa. Kipengee cha kumi cha katiba ya Gabon kinaeleza kuwa rais wa nchi hiyo anapasa kuwa amezaliwa nchini humo. Wapinzani wa Gabon wanasema kuwa ni kweli kwamba Ali Bongo amezaliwa Nigeria na alihamia na kukulia Gabon na kwamba alighushi cheti chake cha kuzaliwa.

Pamoja na hayo yote Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo ilitupilia mbali malalamiko  ya wapinzani kuhusu ugombea wa Ali Bongo katika uchaguzi huu wa leo. Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Gabon iliwatangaza shakhsia 19 kuwa wagombea wa kiti cha urais, hata hivyo wagombea watano kati yao hawakuidhinishwa na tume hiyo kwa kushinda kulipa pesa ya dhamana kiasi cha dola 33,505 za Kimarekani. Wagombea wa kiti cha urais walioidhinishwa wanachuana kwenye uchaguzi wa leo  huku hatua za kiusalama zikiwa zimeimarishwa kote nchini. Hapo kabla ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya ulivitolea wito vyama na makundi ya kisiasa ya upinzani huko Gabon kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi huru na wa kiuadilifu.Tayari pande mbili zinazozozana huko Gabon zimetuhumiana kufanya udanganyifu katika uchaguzi wa leo kwa kununua kadi za kupigia kura. Pamoja na kuwa Gabon ni moja ya nchi tajiri sana barani Afrika, lakini weledi wa mambo wanasema kuwa mgawo wa utajiri wa nchi hiyo usio wa kiuadilifu umesababisha raia wengi wa nchi hiyo kupinga siasa za chama tawala. Vyama vya upinzani vinakituhumu chama tawala kuwa kinajikusanyia utajiri  kwa madhara ya wananchi kwa kuingia mikataba ya muda mrefu na nchi za Magharibi hususan Ufaransa, na hivyo kuzipa fursa ya kupora madini ya nchi hiyo.