Waasi wa Niger Delta nchini Nigeria watoa wito wa kusitishwa mapigano
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i14308-waasi_wa_niger_delta_nchini_nigeria_watoa_wito_wa_kusitishwa_mapigano
Waasi wa eneo la Niger Delta nchini Nigeria wametoa wito wa kusitishwa mapigano katika eneo hilo la kusini mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 30, 2016 23:56 UTC
  • Waasi wa Niger Delta nchini Nigeria watoa wito wa kusitishwa mapigano

Waasi wa eneo la Niger Delta nchini Nigeria wametoa wito wa kusitishwa mapigano katika eneo hilo la kusini mwa nchi hiyo.

Katika barua ya wazi waliyomwandikia Rais Muhammadu Buhari, waasi hao wametaka kuhitimishwa mapigano ya silaha na kutekelezwa usitishaji vita katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Katika barua hiyo imeelezwa kuwa muelekeo chanya na nia njema ya serikali ya Abuja utawezesha kutekelezwa usitishaji vita endelevu katika eneo la Niger Delta.

Wanamgambo wa Niger Delta

Katika barua hiyo kwa Rais Buhari, waasi wa Niger Delta mbali na kutangaza utayari wao wa kufanya mazungumzo na serikali kuhusiana na madai na matakwa yao wameeleza kwamba kutumwa vikosi vya jeshi katika eneo hilo hakutokuwa na tija yoyote.

Barua hiyo ya wanamgambo wa eneo la Niger Delta imeandikwa baada ya Rais wa Nigeria kutoa onyo kwa makundi ya waasi yanayobeba silaha katika eneo hilo kwamba serikali itaamiliana nayo kama inavyoamiliana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram. Buhari alitoa onyo hilo pembeni ya kikao cha "Mkutano wa Kimataifa wa Ustawi wa Afrika".

Rais Muhammadu Buhari (kulia), wanamgambo wa Niger Delta

Wakati huohuo Gavana wa jimbo la Bayelsa, Henry Dickson amesema kutumwa vikosi vya jeshi pekee katika eneo la Niger Delta hakutoshi kwa ajili ya kukabiliana na mashambulio ya makundi ya waasi yanayolenga vinu na mabomba ya mafuta bali inapasa zichukuliwe hatua nyengine za lazima na kwa tahadhari.

Vinu na mabomba ya mafuta yaliyoripuliwa na wabeba silaha Niger Delta

Hii ni katika hali ambayo makundi yanayobeba silaha yameshambulia na kuripua vinu vya gesi katika eneo la Wascravos katika jimbo la Delta kusini mwa Nigeria.../