Kuidhinishwa matokeo rasmi ya uchaguzi wa Rais nchini Gabon
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i14410-kuidhinishwa_matokeo_rasmi_ya_uchaguzi_wa_rais_nchini_gabon
Kamisheni ya Uchaguzi nchini Gabon imemtangaza Rais Ali Bongo kuwa mshindi wa uchaguzi wa Rais uliofanyika tarehe 27 mwezi uliopita na hivyo ataiongoza nchi hiyo ya Kiafrika kwa kipindi kingine cha miaka saba.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 01, 2016 05:21 UTC
  • Kuidhinishwa matokeo rasmi ya uchaguzi wa Rais nchini Gabon

Kamisheni ya Uchaguzi nchini Gabon imemtangaza Rais Ali Bongo kuwa mshindi wa uchaguzi wa Rais uliofanyika tarehe 27 mwezi uliopita na hivyo ataiongoza nchi hiyo ya Kiafrika kwa kipindi kingine cha miaka saba.

Kabla ya hapo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Gabon ilikuwa tayari imemtangaza Ali Bongo kwamba, ndiye aliyeshinda kinyang'anyiro cha Urais. Hata hivyo wapinzani waling'ang'ania kwamba, matokeo hayo yanapaswa kuidhinishwa na Kamisheni ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo. Matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo yanaonyesha kuwa, Ali Bongo ameibuka mshindi kwa kujipatia takribani asilimia 50 ya kura na hivyo kumshinda kwa asilimia mbili tu ya kura mshindani wake mkuu Jean Ping mwanadiplomasia wa zamani na aliyesimama kuchuana na Bongo kwa tiketi ya muungano wa vyama vya upinzani.

Wawakilishi wa vyama vya upinzani walisusia kikao cha Kamisheni ya Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya kuidhinisha matokeo hayo na kutoa wito wa kubandikwa orodha ya kura katika vituo vya kupigia kura. Tofauti ya kura katika majimbo 9 ni kubwa kiasi kwamba, ni vigumu kuyaamini matokeo hayo; kiasi kwamba, hata Faustin Boukoubi shakhsia nambari mbili wa chama tawala nchini humo ametoa wito wa kusambazwa kwa uwazi matokeo ya kura.

Jean Ping, mgombea wa upinzani aliyeshindwa katika uchaguzi wa Gabon

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, Jean Ping mwanasiasa mkongwe ambaye alikuwa mpinzani mkuu wa Rais Ali Bongo katika uchaguzi wa wiki iliyopita bila shaka atataka kuhesabiwa tena kura katika jimbo la Haut –Ogooue linalohesabiwa kuwa ngome ya Ali Bongo. Katika hali ambayo ushiriki wa wapiga kura katika majimbo manane ulikuwa takribani asilimia 60, Kamisheni ya Uchaguzi ya Gabon imetangaza kuwa, ushiriki wa wapiga kura katika jimbo la Haut –Ogooue  ulikuwa asilimia 99.93 na kwamba, Rais Bongo amepata asilimia 95 ya kura katika jimbo hilo.

Wajuzi wa mambo katika duru za kisiasa barani Afrika nao wanakiri kwamba, ni vigumu mno kwa wananchi wa nchi hiyo kuyakubali matokeo hayo. Labda ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana wakazi wa mji mkuu Libreville walimiminika katika mitaa na barabara za mji mkuu huo mara tu baada ya Tume ya uchaguzi kutangaza matokeo hayo wakionyesha kupinga matokeo hayo. Hali hiyo ilipelekea kutokea mapigano kati yao na polisi ya kuzuia fujo na ripoti za awali zinasema watu wawili wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa. Baada ya uchaguzi wa Agosti mwaka 2009 ambapo Ali Bongo alishinda kiti cha Urais na kumrithi baba yake katika uchaguzi uliokuwa na utata, kuliibuka machafuko makubwa ya umwagaji damu.

Machafuko ya Gabon baada ya Rais Ali Bongo kutangazwa mshindi 

Katika kipindi cha miaka saba iliyopita Rais Bongo alifanya juhudi za kuondoka katika kivuli cha baba yake aliyetawala kwa miaka 42 na kuwaonesha wananchi wa Gabon kwamba, ana uwezo yeye kama yeye na sio kwamba, anatumia tu jina la baba yake. Licha ya kuwa alikuwa akiungwa mkono katika kampeni za uchaguzi wa wiki iliyopita na kaumu ya Teke, lakini wapinzani wanaamini kwamba, nafasi aliyonayo Ali Bongo hivi sasa chimbuko lake ni urithi wa kifamilia alioupata kutoka kwa baba yake yaani Omar Bongo. Kwa mtazamo huo tunaweza kusema kuwa, kubakia tena madarakani Ali Bongo huko Gabon hadi mwaka 2023 maana yake ni kuongezwa muda wa kuendelea kutawala familia ya Bongo na kwa ibara nyingine ya wazi zaidi ni kwamba, utawala huo umekuwa ni wa kurithishana.

Hii ni katika hali ambayo, katika kipindi cha utawala wa chama kimoja ambapo Omar Bongo aliiongoza nchi hiyo kwa miaka 42 hadi alipofariki dunia mwaka 2009, wananchi wa nchi hiyo walikuwa wakiutambua utawala wake kuwa ni wa kidikteka na uliogubikwa na ufisadi. Ikumbwe kuwa, katika kipindi cha miongo minne iliyopita, Ali Bongo alishika nyadhifa muhimu  kama mshauri wa kisiasa, Waziri wa Mashauri ya Kigeni na Waziri wa Ulinzi katika baraza la mawaziri la baba yake na hadi baba yake anaaga dunia Ali Bongo alikuwa mmoja wa viongozi muhimu nchini humo. 

Katika uchaguzi wa mara hii pia, licha ya kuweko upinzani ndani ya chama tawala cha Democratic Party Ali Bongo alitangaza nia ya kugombea kiti cha Urais kwa mara ya pili. Ali Bongo ameshika tena hatamu za uongozi wa Gabon kupitia uchaguzi uliojaa utata ambapo mbali na malalamiko ya vyama vya upinzani, na Umoja wa Ulaya, hata Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa ambayo ni mmoja wa waitifaki wakongwe wa Gabon nayo imepaza sauti kulalamikia matokeo ya uchaguzi huo. Bila shaka malalamiko hayo yatakuwa ni wenzo wa kumshinikiza Rais Ali Bongo na chama chake tawala cha Demcratic Party.