Wanajeshi wanalinda doria Gabon kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi
Wanajeshi wanalinda doria katika mji mkuu wa Gabon, Libreville baada ya siku mbili za machafuko baada ya wapinzani kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais.
Ijumaa ya leo pia wananchi walionekana wakijitokeza tena mitaani baada ya utulivu wa wastani kurejea huku wengi wakimiminika madukani kununua bidhaa muhimu.
Watu watatu wamepoteza maisha katika ghasia hizo huku wengine zaidi ya 1,000 wakitiwa mbaroni baada ya wafuasi wa mgombea urais aliyeshindwa, Jean Ping kuandamana kupinga matokea ya uchaguzi.
Siku ya Jumatano, Tume ya Uchaguzi ya Gabon ilimtangaza Rais Ali Bongo kuwa mshindi na hivyo kumuwezesha kuendeleza kwa miaka mingine saba utawala wa nusu karne wa familia yake katika nchi hiyo ya kati mwa Afrika yenye utajiri wa mafuta.
Ping, muitifaki wa zamani wa Bongo, amemtaka rais huyo aondoke madarakani. Bongo alitangazwa mshindi kwa asilimia 49.80 ya kura zilizopigwa Jumamosi iliyopita huku Ping akipata asilimia 48.23.