Wanamgambo wa al-Shabab wauawa katika operesheni ya jeshi la Somalia Baidoa
Vikosi vya usalama vya Somalia vimefanya operesheni kubwa dhidi ya wanamgambo wa kigaidi wa al-Shabab katika eneo la kusini magharibi mwa nchi hiyo.
Operesheni hiyo ya kijeshi katika mji wa Baidoa imepelekea kwa uchache wanamgambo wanne wa kundi la kigaidfi la al-Shabab kuuawa na wengine kadhaa kutiwa mbaroni.
Vikosi vya usalama vya Somalia vimetangaza kuwa, kamanda wa wangambo wa al-Shabab katika eneo la Bay katika mji wa Bakool ni miongoni mwa wanachama wa al-Shabab waliotiwa mbaroni na vikosi vya usalama vya nchi hiyo.
Wanamgambo wa al Shabab wamekuwa wakivuruga hali ya usalama huko Somalia kwa kutekeleza mashambulizi katika maeneo mbalimbali nchini humo na hata dhidi ya kikosi cha kulinda amani nchini humo (AMISOM).
Vikosi vya pamoja vya Somalia na vile vya kusimamia amani vya Umoja wa Afrika AMISOM vimefanikiwa kulifurusha kundi hilo la kitakfiri katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na katika miji mingine mikubwa ya nchi hiyo, lakini wanamgambo wake wanaendelea kufanya mashambulio ya hapa na pale katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Tume ya Uchaguzi ya Somalia imetangaza kuwa uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo utafanyika tarehe 30 Oktoba na wa bunge umepangwa kufanyika kati ya tarehe 24 Septemba hadi tarehe 10 Oktoba.