Asasi zisizo za kiserikali zaonya juu ya kutokea maafa ya kibinadamu Nigeria
Asasi zisizo za kiraia zimetahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea maafa ya kibinadamu kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Asasi hizo zisizo za kiserikali ikiwemo ya Madaktari Wasio na Mipaka zimetoa taarifa ambayo sambamba na kutahadharisha kuhusiana na kutokea maafa ya kibinadamu nchini Nigeria zimetangaza kuwa, kuanzia mwaka jana hadi sasa maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria takribani yamekuwa yakikabiliwa na ukame.
Asasi hizo zimesema bayana katika taarifa yao kwamba, katika aghalabu ya kambi za wakimbizi katika jimbo la Borno hali ya mambo ni ya kutia wasiwasi mno. Taarifa hiyo aidha imeeleza kwamba, asasi zisizo za kiserikali zimechukua hatua kadhaa za kuboresha hali ya mambo lakini hatua hizo hazijaweza kusaidia.
Jumuiya hizo zimesema kwamba, hali ya kibinadamu katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria ni mbaya mno na kwamba, kama hakutachukuliwa hatua za maana kwa ajili ya kukabiliana na hali hiyo basi kuna uwezekano maeneo hayo yakakumbwa na maafa ya kibinadamu.
Hali ya lishe duni baina ya watoto katika jimbo la Borno imefikia kiwango kibaya mno na kuendelea kwa hali hiyo kutapelekea watoto wengi kupoteza maisha, imebainisha sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya asasi hizo zisizo za kiserikali.
Ikumbukwe kuwa, maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria yamekuwa yakishuhudia harakati za kundi la kigaidi la Boko Haram ambazo zimepanuka na kufika katika nchi jirani za Niger, Cameroon na Chad na hivyo kusababisha hali ya maisha katika maeneo hayo kuwa ngumu.