Jeshi la Nigeria lawakamata wanamgambo wa Avengers
Jeshi la Nigeria limetangaza kuwakamata wanamgambo wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi la Niger Delta Avengers (NDA) yaani Walipizaji Kisasi wa Niger Delta.
Jeshi la Nigeria limetnagaza kumkamata mkuu wa NDA Issac Romeo pamoja na wafuasi wake hivi karibuni katika mji mkuu wa Jimbo la Cross River, Calabar, katika eneo la Delta.
Wanamgambo hao wamekamatwa pamoja na kuwa walitangaza usitishwaji vita na vikosi vya serikali mwaka jana. Jeshi linahofia kuwa yamkini NDA wakaanzisha hujuma dhidi ya vituo vya kuzalisha mafuta na gesi wakati wa mazungumzo ya Amani. Kundi la NDA lilitangaza uwepo wake Mwezi Machi na limekuwa likihujumu vituo vya kuzalisha mafuta na gesi hasa mabomba katika eneo la Delta. Kundi hilo linataka wakaazi wa eneo hilo wafaidike na utajiri mkubwa wa mafuta na gesi iliyopo katika ardhi yao.
Eneo la Niger Delta liko kusini mwa Nigeria na lina majimbo tisa ambayo yanaongoza kwa hifadhi ya mafuta nchini humo.
Ni miongo minne sasa tokea Nigeria ivumbue mafuta na ianze kuyachimba na kuyauza katika masoko ya kimataifa. Lakini Wanigeria hawajafaidika ipasavyo na utajiri huo wa kitaifa wa nchi yao.
Nigeria kwa muda mrefu imekuwa mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta ghafi ya petroli barani Afrika. Lakini wakaazi takribani milioni 186 wa nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika bado wanaishi katika umasikini mkubwa.