Kikosi cha AMISOM chadhibiti ngome muhimu ya al-Shabab nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i14992-kikosi_cha_amisom_chadhibiti_ngome_muhimu_ya_al_shabab_nchini_somalia
Kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kimefanikiwa kudhibiti ngome muhimu ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la al-Shabab katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Sep 09, 2016 10:10 UTC
  • Kikosi cha AMISOM chadhibiti ngome muhimu ya al-Shabab nchini Somalia

Kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kimefanikiwa kudhibiti ngome muhimu ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la al-Shabab katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Msemaji wa kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM ametangaza kuwa, kikosi hicho kikisaidiana na jeshi la Somalia kimedhibiti moja ya ngome muhimu za wanamgambo wa al-Shabab katika eneo la Abdalla Birole kusini mwa nchi hiyo.

Luteni Kanali Joe Kibet ameongeza kuwa, wanachama wa kundi la al-Shabab katika eneo la Abdalla Birole wamelikimbia eneo hilo.

Wanamgambo wa al-Shabab

Aidha amesema, hakuna askari wa kikosi cha AMISOM au wa jeshi la Somalia aliyeuawa au kujeruhiwa katika operesheni ya kulikomboa eneo hilo kutoka mikononi mwa wanamgambo wa al-Shabab. katika siku za hivi karibuni kikosi cha AMISOM kikishirikiana na jeshi la Somalia vimepata mafanikio makubwa katika vita vyao dhidi ya wanamgambo wa al-Shabab. Mafanikio hayo yanaelezwa kuwa ni ya mahala pake hasa katika kipindi hiki ambacho Somalia inajiandaa na uchaguzi wa Bunge na Rais.

Tume ya Uchaguzi ya Somalia imetangaza kuwa, uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo utafanyika tarehe 30 Oktoba na wa bunge umepangwa kufanyika kati ya tarehe 24 Septemba hadi tarehe 10 Oktoba.

Askari wa AMISOM Somalia

Wanamgambo wa al Shabab wamekuwa wakivuruga hali ya usalama huko Somalia kwa kutekeleza mashambulizi katika maeneo mbalimbali nchini humo na hata dhidi ya kikosi cha kulinda amani nchini humo (AMISOM).  

Askari wa Umoja wa Afrika wapo nchini Somalia kwa lengo la kuisadia serikali ya nchi hiyo katika vita vyake dhidi ya wanachama wa kundi hilo maarufu kwa kutenda jinai dhidi ya binaadamu.