Usalama waimarishwa Somalia kabla ya kuanza kikao cha viongozi wa IGAD
Serikali ya Somalia imechukua hatua kali za kuimarisha usalama katika mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu sambamba na kukaribia kufanyika kikao cha viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ustawi wa Mashariki mwa Afrika IGAD
Rais Hassan Sheikh Mohamoud ametangaza kuwa ulinzi umeimarishwa katika mji mkuu Mogadishu na maeneo ya kandokando yake sambamba na kukaribia kikao cha viongozi wa nchi wanachama wa IGAD kinachotazamiwa kufanyika siku ya Jumanne.
Rais wa Somalia amefafanua kuwa viongozi wa nchi nane wanachama wa jumuiya hiyo ya ustawi ya kieneo ambazo ni Djibouti, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia yenyewe, Sudan Kusini, Sudan na Uganda wanatazamiwa kuhudhuria kikao hicho.
Mojawapo ya ajenda zinazotazamiwa kutawala kikao hicho ni mafanikio ya kisiasa na kiusalama yaliyopatikana nchini Somalia na uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliopangwa kufanyika mnamo mwezi huu wa Septemba na ujao wa Oktoba.
Japokuwa vikosi vya jeshi la Somalia vikisaidiwa na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika (AMISOM) vimefanikiwa kuwatimua wapiganaji wa kundi la kigaidi la Al-Shabab katika mji mkuu Mogadishu, lakini kundi hilo la kitakfiri lingali linaendelea kufanya mashambulio dhidi ya taasisi za serikali na katika maeneo ya umma.
Hivi sasa kuna askari wapatao 22,000 wa AMISOM wanaoisaidia serikali ya Somalia kupambana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Al-Shabab na kurejesha amani nchini humo.
Mbali na kadhia ya Somalia, viongozi wa nchi wanachama wa IGAD wanatazamiwa kuchunguza pia njia za kuhatimisha mgogoro unaoendelea nchini Sudan Kusini.../