Usalama waimarishwa Somalia kabla ya mkutano wa kilele wa IGAD
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i15157-usalama_waimarishwa_somalia_kabla_ya_mkutano_wa_kilele_wa_igad
Serikali ya Somalia imeimarisha usalama kote katika nchi hiyo, hususan mji mkuu Mogadishu, wakati wa kufanyika kwa mkutano wa Shirika la Maendeleo la Kiserikali la Nchi za Afrika Mashariki IGAD mjini humo hapo kesho
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Sep 12, 2016 02:20 UTC
  • Usalama waimarishwa Somalia kabla ya mkutano wa kilele wa IGAD

Serikali ya Somalia imeimarisha usalama kote katika nchi hiyo, hususan mji mkuu Mogadishu, wakati wa kufanyika kwa mkutano wa Shirika la Maendeleo la Kiserikali la Nchi za Afrika Mashariki IGAD mjini humo hapo kesho

Katika kuhakikisha mkutano huo unafanyika kwa amani, Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM jana kiliwakamata wataalamu wawili wa mabomu wa kundi la Al-Shabaab katika sehemu ya kusini nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na kikosi hicho imesema, watu hao walikamatwa katika operesheni ya usalama iliyofanyika karibu na mji wa Kismayu.

Viongozi kutoka nchi nane wanachama wa IGAD yaani Djibouti, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda wanatazamiwa kushiriki katika mkutano huo wa kilele.

Askari wa AMISOM wakilinda doria Mogadishu

 

Mkutano huo unatazamiwa kujadili mafanikio ya kiusalama na kisiasa Somalia na uchaguzi mkuu ujao ambao umepangwa kufanyika mwezi huu wa Septemba na mwezi ujao wa Oktoba nchini humo. Mkutano huo wa Mogadishu pia unatazamiwa kujadili njia za kumaliza mgogoro wa Sudan Kusini.

Waziri wa Mambo ya Nje ya Somalia Abdisalam Omar Hadliye amesema mkutano huo wa IGAD utakuwa wa kwanza wa kiwango hicho cha kimataifa kufanyika tangu nchi hiyo ikumbwe na vita katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili.

Kuna askari zaidi ya elfu 22 wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika Somalia maarufu kama AMISOM ambao wametoa pigo kubwa kwa magaidi wa kundi la Al Shabab sambamba na kurejesha amani ya wastani katika nchi hiyo.