Viongozi wa Jumuiya ya IGAD wasisitiza kufanyika uchaguzi huru nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i15286-viongozi_wa_jumuiya_ya_igad_wasisitiza_kufanyika_uchaguzi_huru_nchini_somalia
Viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kieneo ya Mashariki mwa Afrika IGAD wameitaka serikali ya Somalia kufanya uchaguzi huru na wenye itibari nchini humo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Sep 14, 2016 03:21 UTC
  • Viongozi wa Jumuiya ya IGAD wasisitiza kufanyika uchaguzi huru nchini Somalia

Viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kieneo ya Mashariki mwa Afrika IGAD wameitaka serikali ya Somalia kufanya uchaguzi huru na wenye itibari nchini humo.

Viongozi hao ambao walikutana jana katika mkutano wa siku moja mjini Mogadishu mji mkuu wa Somalia wamesisitiza kwamba, serikali ya nchi hiyo inapaswa kufanya uchaguzi huru na wa wazi.

Taarifa taarifa ya mwishoni mwa kikao hicho imetaka wananchi wa Somalia kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika uchaguzi ujao wa Bunge na Rais. 

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alipowasili Mogadishu kushiriki mkutano wa IGAD

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Somalia uchaguzi wa Bunge utafanyika tarehe 24 mwezi huu hadi Oktoba 10 mwezi ujao huku ule wa Rais ukitarajiwa kufanyika tarehe 30 ya mwezi ujao.

Aidha viongozi hao wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kieneo ya Mashariki mwa Afrika IGAD wametoa hakikisho kuwa, jamii ya kimataifa iko tayari kuisadia Somalia, kuhakikisha kuwa uchaguzi ujao unafanyika kwa wakati kwa mujibu wa matakwa ya wananchi wa Somalia.

Kuhusiana na zoezi la kurejeshwa wakimbizi wa Somalia kutoka nchini Kenya ambalo limekuwa likiendelea, viongozi hao sasa wametoa wito wa kutaka kufanyika zoezi hilo kwa njia ya amani.

Bango la kukaribisha washiriki wa mkutano wa IGAD Mogadishu

Kikao hicho cha IGAD mjini Mogadishu kimetajwa kuwa cha kihistoria kutokana na kuwa hii mara ya kwanza kwa mkutano kama huo kufanyika mjini Mogadishu tangu kuanzishwa kwa jumuiya hiyo. 

Marais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn na mwenyeji Rais Hassan Sheikh Muhammoud wa Somalia walihudhuria kikao hicho.