Waziri wa masuala ya wakimbizi wa Uganda atembelea Burundi
Waziri wa Nchi wa serikali ya Uganda katika masuala ya wakimbizi, Musa Ecweru, amefanya ziara nchini Burundi kwa lengo la kujadili masuala ya wakimbizi wa nchi hiyo.
Térence Ntahiraja, msemaji wa Wizara ya Mambo ya ndani ya Burundi amesema kuwa Musa Ecweru aliwasili nchini humo jana Jumatano akiandamana na ujumbe maalumu ikiwa ni kuitikia mwito wa Pascal Barandagiye, waziri mwenzake wa Burundi. Akiashiria kutoeleweka idadi ya wakimbizi wa Burundi walioko nchini Uganda, Térence Ntahiraja amesema ana matumaini kuwa katika safari hiyo ya Ecweru nchini Burundi hilo ndilo jambo litakalojadiliwa na viongozi wa pande mbili.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Burundi ameongeza kuwa, safari ya Musa Ecweru nchini humo ni fursa nzuri kwa ajili ya kuchunguza masuala shirikishi na kuinua kiwango cha ushirikiano baina yao. Kadhalika amesema kuwa, katika safari hiyo, Burundi na Uganda zitazungumzia suala la kurejea nyumbani kwa hiari wakimbizi wa Burundi walioko nchini Uganda. Kwa mujibu wa viongozi wa Burundi, zaidi ya Warundi laki mbili walikimbilia nchi jirani za Rwanda, Tanzania, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, baada ya kushadidi machafuko ya kisiasa nchi mwao. Kadhalika Burundi inaamini kwamba, karibu wakimbizi elfu 90 elfu wa nchi hiyo waliokuwa nchi jirani tayari wamerejea makwao kwa hiari hadi sasa.