Wahanga wa machafuko ya baada ya uchaguzi Kodivaa walipwa fidia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i15355-wahanga_wa_machafuko_ya_baada_ya_uchaguzi_kodivaa_walipwa_fidia
Waziri wa Masuala ya Mshikamano wa Kijamii wa Ivory Coast amesema kuwa, serikali ya nchi hiyo itaendelea kuwalipa fidia wahanga wa machafuko ya baada ya uchaguzi wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 15, 2016 07:25 UTC
  • Profesa Mariatou Koné, Waziri wa Masuala ya Mshikamano wa Kijamii wa Ivory Coast
    Profesa Mariatou Koné, Waziri wa Masuala ya Mshikamano wa Kijamii wa Ivory Coast

Waziri wa Masuala ya Mshikamano wa Kijamii wa Ivory Coast amesema kuwa, serikali ya nchi hiyo itaendelea kuwalipa fidia wahanga wa machafuko ya baada ya uchaguzi wa nchi hiyo.

Profesa Mariatou Koné alisema hayo jana na kuongeza kuwa, karibu wahanga elfu tatu wa mgogoro wa kisiasa wa Kodivaa ya miaka 1990 hadi 2011 wameshalipwa fidia.

Ameongeza kuwa, karibu watu 260 waliojeruhiwa kwenye machafuko ya baada ya uchaguzi katika maeneo tofauti ya Ivory Coast hivi sasa wanapatiwa matibabu maalumu na serikali kwa amri ya Rais Alassane Ouattara, na hali zao zinaendelea vizuri.

Wahanga wakuu wa machafuko ni wanawake na watoto wadogo

 

Waziri wa Masuala ya Mshikamano wa Kijamii ya Kodivaa ameongeza kuwa, kumefunguliwa mfuko maalumu wa kuwasaidia wahanga wa masuala mbalimbali nchini humo ujulikanayo kwa jina la mfuko wa FCFA.

Mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1999, uasi wa kutumia silaha wa mwaka 2002 na mgogoro wa baada ya chaguzi za miaka 2010 na 2011 ambayo yalipelekea watu 3000 kuuawa, ni miognoni mwa migogoro iliyoikumba nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.