Burundi: Raia wetu waliokimbia nchi kwa machafuko wanaendelea kurudi kwa hiari
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i15391-burundi_raia_wetu_waliokimbia_nchi_kwa_machafuko_wanaendelea_kurudi_kwa_hiari
Serikali ya Burundi imesema kuwa, hadi sasa zaidi ya wakimbizi elfu 30 raia wa nchi hiyo wamerejea makwao katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 15, 2016 23:31 UTC
  • Burundi: Raia wetu waliokimbia nchi kwa machafuko wanaendelea kurudi kwa hiari

Serikali ya Burundi imesema kuwa, hadi sasa zaidi ya wakimbizi elfu 30 raia wa nchi hiyo wamerejea makwao katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni.

Hayo yamesemwa na Pascal Barandagiye, Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Burundi na kuongeza kuwa jumla ya wakimbizi elfu 31 na 826 wamereja makwao eneo la kusini nchini humo kutoka Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya na Malawi. Barandagiye aliyasema hayo katika kikao na Musa Ecweru, Waziri wa Nchi wa serikali ya Uganda katika Masuala ya Wakimbizi aliyefanya safari nchini Burundi na kusema kuwa, kurejea wakimbizi hao makwao ni kwa hiari na kwamba, tangu mwezi Januari mwaka huu karibu wakimbizi 85 elfu walikuwa tayari wamerejea nchini.

Musa Ecweru, Waziri wa Nchi wa serikali ya Uganda katika Masuala ya Wakimbizi

Safari ya Waziri wa Nchi wa serikali ya Uganda katika Masuala ya Wakimbizi imefanyika kufuatia mwito wa serikali ya Bujumbura kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu raia wa Burundi walioko nchini Uganda ambao idadi yao inakaribia elfu 31. Burundi ilitumbukia katika wimbi la machafuko hapo mwezi Aprila mwaka jana, baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumwidhinisha Rais Pierre Nkurunziza kugombea muhula wa tatu mfululizo katika uchaguzi wa rais uliopita.