Sudan Kusini yailaumu Marekani kwa kuendelea kuiwekea vikwazo
Serikali ya Sudan Kusini imeilaumu Marekani kwa siasa zake zisizo sahihi kuhusiana na nchi hiyo na kusema, Juba inahitajia misaada mbalimbali ikiwemo ya silaha na si vikwazo.
Makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Taban Deng Gai ameliambia shirika la habari la AFP pambizoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kwamba, wananchi wa nchi hiyo wamechoshwa na machafuko, hivyo wanahitajia misaada ya kila namna.
Amedai kuwa, vita vimeshaisha nchini humo na kwamba anasema kwa kujiamini kuwa Sudan Kusini sasa iko katika amani na serikali iko katika mchakato wa kurejea katika kazi zake za kawaida. Hata hivyo amesema, nchi kama Marekani zinafanya mambo ambayo yanalenga kuharibu hali hiyo. Amehoji kwa kusema: Kwa nini hali hiyo ivurugwe.
Wamarekani wanapaswa kutusaidia kutia nguvu polisi wetu na kuimarisha jeshi letu la ulinzi na sio kutuwekea vikwazo ambavyo vinazidisha hali kuwa mbaya nchini mwetu. Hata hivyo, Ban Ki moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anataka serikali ya Sudan Kusini itoe ushirikiano zaidi kwa maafisa wa umoja huo ili aweze kuitetea Juba katika ripoti yake kwa Baraza la Usalama mwezi ujao.
Wakati huo huo shirika la habari la Ufaransa limeandika, ni vigumu kusema kwamba hali imerejea kuwa ya kawaida nchini Sudan Kusini. Mapigano ya miaka miwili na nusu nchini humo yameua makumi ya maelfu ya watu na kuwakosesha makazi zaidi ya milioni mbili na nusu wengine.
Zaidi ya wakimbizi milioni moja wanaishi katika mazingira mabaya kwenye kambi za wakimbizi. Aidha kuna kesi nyingi za uvunjaji wa haki za binadamu kama vile kunajisiwa wawanawake na wasichana nchini Sudan Kusini.
Mapigano nchni humo yalizuka mwezi Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu makamu wake wakati huo, Riek Machar kwamba amepanga njama za kumpindua.