Kiongozi wa kundi la Niger Delta atiwa mbaroni Nigeria
Kamanda wa kikosi cha baharini nchini Nigeria ametangaza kuwa kiongozi wa kundi la waasi la Niger Delta, kusini mwa nchi hiyo ametiwa nguvuni.
Joseph Dzunve, ambaye anaongoza kikosi cha baharini kinachoendesha operesheni za kijeshi katika jimbo la Delta, kusini mwa Nigeria amesema kuwa, katika operesheni za kurejesha amani eneo hilo, askari wamefanikiwa kumtambua na kumtia mguvuni Ibrahim Sorou, kiongozi wa kundi hilo. Dzunve ameongeza kuwa, hadi sasa jeshi hilo linaendeleza juhudi za kulimaliza kabisa kundi hilo la waasi na kwamba, Nigeria imeazimia kupambana na magendo ya mafuta na mashambulizi ya waasi dhidi ya taasisi za mafuta nchini humo.
Kadhalika kamanda huyo wa kikosi cha baharini katika jimbo la Delta amesema kuwa, hadi sasa jeshi hilo limeweza kuharibu vituo 74 vya uzalishaji na uuzaji mafuta ya magendo vilivyokuwa vinamilikiwa na waasi sanjari na kudhibiti kiasi kikubwa cha silaha. Kundi la waasi la Niger Delta lilianzisha wimbi la mashambulizi mwezi Februari mwaka huu kwa kuyalenga mashirika ya mafuta ya petroli ya serikali na ya kigeni kusini mwa Nigeria. Waasi hao pia wanamtuhumu Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo kuwa hajali maslahi ya wananchi wa eneo hilo lenye utajiri wa mafuta.