Mamia ya maelfu ya wakimbizi wa Burundi wahajiri katika nchi jirani
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa mamia ya maelfu ya wakimbizi wa Burundi wamehamia katika nchi jirani.
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limeripoti kuwa wakimbizi wa Burundi laki tatu wamehajiri huko Tanzania, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda na Zambia. Wakimbizi hao wa Burundi wameamua kuhajiri katika nchi jirani wakikimbia mchafuko, vitisho, mateso na vitendo vya utekaji nyara vinavyojiri nchini kwao. Ripoti ya UNHCR imeongeza kuwa hivi sasa Tanzania imewapa hifadhi wakimbizi wa Burundi 163,000, Uganda wakimbizi 41,000, Rwanda ikiwa na wakimbizi wa Burundi zaidi ya 81,000, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakimbizi zaidi ya 21,000 na Zambia ikiwahifadhi wakimbizi wa Burundi 1700.
Ghasia na machafuko yalianza huko Burundi tangu mwezi Aprili mwaka jana na kisha hali hiyo ilishtadi baada ya Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kuamua kugombea kiti cha urais kwa muhula wa tatu. Wapinzani Burundi walipinga na kuilalamikia pakubwa hatua hiyo ya Rais Nkurunziza jambo lililosababisha maandamano ya mitaani huko Burundi . Hatimaye Rais Nkurunziza alishinda uchaguzi wa mwaka jana hatua iliyosabisha machafuko yaliyopelekea kuuawa watu wengi na kuwalazimisha mamia ya maelfu ya wengine kukimbilia katika nchi jirani kuepuka machafuko.