Walipiza Kisasi Niger Delta watangaza kuhujumu kituo cha mafuta
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16024-walipiza_kisasi_niger_delta_watangaza_kuhujumu_kituo_cha_mafuta
Kundi la wanamgambo wa Nigeria wanaojiita Niger Delta Avengers yaani Walipiza Kisasi wa Niger Delta wametangaza kutekeleza hujuma ya kwanza dhidi ya kituo cha uzalishaji mafuta kusini mwa nchi hiyo kwa mara ya kwanza tangu watangaze kusitisha hujuma mwezi Agosti.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 25, 2016 04:28 UTC
  • Walipiza Kisasi Niger Delta watangaza kuhujumu kituo cha mafuta

Kundi la wanamgambo wa Nigeria wanaojiita Niger Delta Avengers yaani Walipiza Kisasi wa Niger Delta wametangaza kutekeleza hujuma ya kwanza dhidi ya kituo cha uzalishaji mafuta kusini mwa nchi hiyo kwa mara ya kwanza tangu watangaze kusitisha hujuma mwezi Agosti.

Katika taarifa Jumamosi, wanamgambo hao wamesema kuwa, Ijumaa usiku walihujumu bomba la Bonny ambalo husafirisha mafuta nje ya nchi. Wanamgambo hao wamesema walisitisha shughuli za bomba lenye upana wa nchi 48 kupitia hujuma hiyo.

Walipiza kisasi wa Niger Delta wanataka wakaazi wa eneo la Niger Delta wafaidike na utajiri mkubwa wa mafuta ghafi ya petrol yanayochimbwa eneo hilo. Wanasema hujuma yao mpya inalenga 'kuimasha' serikali kwani imekuwa ikiwatisha vijana wa eneo hilo tokea usitishwaji vita utangazwe eneo hilo.

Wanamgambo wa Niger Delta

Wakaazi wa eneo la Delta, ambao baadhi yao wanayaunga mkono makundi ya wanamgambo, wamekuwa kwa muda mrefu wakilalamikia hali ya umasikini ya eneo lao hilo ambalo linazalisha mafuta yanayodhamini asilimia 70 ya pato lote la taifa la Nigeria.

Wanamgambo wa eneo hilo la Niger Delta wanamtuhumu Rais Muhammadu Buhari kwa kutojali maslahi ya wananchi wa nchi hiyo.