Mahakama ya Katiba ya Gabon yaaidhinisha matokeo ya uchaguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16027-mahakama_ya_katiba_ya_gabon_yaaidhinisha_matokeo_ya_uchaguzi
Mahakama ya Katiba ya Gabon imeidhinisha matokeo ya uchaguzi wa rais wa hivi karibuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 25, 2016 04:45 UTC
  • Mahakama ya Katiba ya Gabon yaaidhinisha matokeo ya uchaguzi

Mahakama ya Katiba ya Gabon imeidhinisha matokeo ya uchaguzi wa rais wa hivi karibuni.

Mahakama hiyo juzi Ijumaa iliidhinisha ushindi wa Ali Bongo Ondimba katika uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 27 Agosti mwaka huu. Kwa utaratibu huo, Mahakama ya Katiba ya Gabon imetupilia mbali dai la Jean Ping mgombea wa kiti cha urasi aliyeshindwa kwenye uchaguzi huo. Mahakama ya Katiba ya Gabon ilifafanua  kuwa takwa la kuhesabiwa upya kura katika mkoa wa Haut- Ogooue ambako Ali Bongo anatoka  ni jambo lilisokubalika. Kabla ya hapo, wapinzani waliomba kuhesabiwa upya kura za uchaguzi katika mkoa huo. Kwa msingi huo, Ali Bongo Ondimba amechaguliwa kuwa Rais wa Gabon kwa duru nyingine moja ya miaka saba. Matokeo ya uchaguzi wa rais ya nchi hiyo yanaonyesha kuwa,  Ali Bongo ameshinda uchaguzi wa Rais kwa kupata asilimia 49 za kura akimpita hasimu wake mkuu Jean Ping aliyepata asilimia 48.

Mahakama ya Katiba ya Gabon jana ilitoa uamuzi huo ambapo Jean Ping mgombea aliyeshindwa kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais nchini humo alikuwa tayari amezungumzia ombi lake la kufuatiliwa kesi ya uchaguzi huo kwenye Mahakama ya Katiba.  Ping aliyataja matokeo ya uchaguzi katika masaa ya awali ya kuanza kuhesabiwa kura kuwa ni ya uchakachuaji na kuyapinga. Mwanadiplomasia huyo alikuwa na matarajio haya kwamba utawala wa Bongo ungeweza kuhitimishwa huko Gabon nchi tajiri kwa mafuta kwa uamuzi ambao ungetolewa na mahakama.

Jeam Ping mwanadiplomasia mtajika aliyedai kuchakachuliwa matokeo ya uchaguzi wa  rais wa Gabon

Mivutano ya kisiasa imepamba moto Gabon tangu kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais. Wapinzani wa Bongo wakiongozwa na wafuasi wa Jean Ping walimiminika  mitaani na kuandamana katika maeneo mbalimbali ya nchi wakidai kuwa, matokeo ya uchaguzi  yaliyotangazwa ni ya uchakachuaji. Maandamano na ghasia hizo ziliingiliwa kati na vikosi vya jeshi na hali ya mambo kuzidi kuwa mbaya ambapo watu zaidi ya 50 waliuliwa. Kushtadi ghasia na machafuko hayo kulizipelekea pande zote mbili kuamua kuwa, malalamiko yaliyopo yafuatiliwe kisheria. Matatizo ya kiuchumi, mivutano ya kisiasa na kukosekana uhuru wa kisiasa na kijamii, ni moja ya masuala ambayo yamekuwa yakikosolewa na wapinzani huko Gabon; huku wakitaka  kuasisiwa demokrasia nchini humo.

Wapinzani wa Ali Bongo wanaamini kuwa, Gabon itaelekea kuwa nchi ya kidikteta iwapo kiongozi huyo ataendelea kusalia uongozini. Wapinani hao wanamtuhumu Ali Bongo kuwa anazipendelea nchi za Magharibi.  Rais wa Gabon amewaita wapinzani kwenye mazungumzo baada ya kuidhinishwa ushindi wake na Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo hapo juzi. Akiwahutubia kupitia televisheni ya taifa, Rais Ali Bongo ameeleza kuwa serikali inawatolea wito wa kujongea kwenye mazungumzo ya kisiasa  viongozi wote wa kisiasa, wakiwemo wagombea walioshindwa katika uchaguzi wa Agosti 27. Gabon hivi sasa iko katika hali ya kuyumbayumba kufuatia uamuzi huo rasmi wa Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo wa kuidhinisha ushindi wa Ali Bongo. Weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa hatua hiyo inaweza kuibua tena machafuko nchini humo hata kama Ali Bongo amewatolea wito wapinzani wa kufanya mazungumzo.