Waislamu wa Nigeria waipa muhula serikali kumuachilia huru Sheikh Zakzaky
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16189-waislamu_wa_nigeria_waipa_muhula_serikali_kumuachilia_huru_sheikh_zakzaky
Waislamu nchini Nigeria wameipa serikali ya nchi hiyo muhula wa wiki moja kuhakikisha inamuachilia huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa harakati ya Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 27, 2016 11:08 UTC
  • Waislamu wa Nigeria waipa muhula serikali kumuachilia huru Sheikh Zakzaky

Waislamu nchini Nigeria wameipa serikali ya nchi hiyo muhula wa wiki moja kuhakikisha inamuachilia huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa harakati ya Kiislamu.

Waislamu wametoa muhula huo kupitia maandamano yaliyofanyika mjini Abuja, mji mkuu wa Nigeria ambapo mbali na kutaka kuachiliwa huru kiongozi huyo wa Kiislamu, wameitaka pia kuchukua hatua za maana kwa ajili ya hali ya kiafya ya shakhsia huyo. Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria imesisitiza kuwa, endapo serikali hiyo haitatekeleza matakwa yao katika muda ulioainishwa, basi itashadidisha maandamano ya nchi nzima dhidi ya serikali hiyo.

Sheikh Ibrahim Zakzaky

Hii ni katika hali ambayo siku za hivi karibuni Waislamu nchini humo wamekuwa wakifanya maandamano wakitaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, mke wake na makumi ya Waislamu ambao wameendelea kushikiliwa na vyombo vya serikali kwa miezi kadhaa sasa na bila kushtakiwa. Aidha Waislamu wanataka kuhitimishwa mienendo isiyo ya kibinaadamu ya jeshi na maafisa usalama wa nchi hiyo dhidi ya Waislamu hususan wa Kishia. Maandamano hayo ya amani dhidi ya serikali yanajiri katika hali ambayo asasi mbalimbali za haki za binaadamu kwa mara kadhaa zimeelezea hali mbaya ya kiafya ya kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu katika korokoro ya serikali. Kwa mujibu wa weledi wa mambo, lengo la serikali ya Rais Muhammadu Buhari ya kumtia mbaroni Sheikh Ibrahim Zakzaky ni kufuta Harakati ya Kiislamu nchini humo, suala linaloonekana kugonga mwamba hadi sasa.