Mjumbe wa UN alaani mauaji ya mwandishi habari Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16282-mjumbe_wa_un_alaani_mauaji_ya_mwandishi_habari_somalia
Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Michael Keating amelaani vikali mauaji ya mwandishi wa habari wa Radio Shabelle Abdiaziz Mohamed Ali yaliyotekelezwa Jumanne na watu wasiojulikana mjini Mogadishu Somalia.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Sep 29, 2016 01:08 UTC
  • Mjumbe wa UN alaani mauaji ya mwandishi habari Somalia

Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Michael Keating amelaani vikali mauaji ya mwandishi wa habari wa Radio Shabelle Abdiaziz Mohamed Ali yaliyotekelezwa Jumanne na watu wasiojulikana mjini Mogadishu Somalia.

Mohammad Ali ambaye alikuwa mwandishi  na ripota mashuhuri, amekuwa mwandishi wa pili kuuawa kikatili mwaka huu nchini Somalia. Kwa mujibu wa mpango wa umoja wa Mataifa nchini Somalia UNSOM, jumla ya waandishi wa habari 31 wameuawa nchini Somalia tangu mwezi Agosti mwaka 2012. Aidha wabunge 18 wameuawa Somalia katika kipindi hicho.

Keating amesema Ali alikuwa mwandishi mwenye ujuzi na utaalamu wa kutosha aliyekuwa akiripoti mikutano mbalimbali ya jumuiya ya kimataifa mjini Moghadishu, na kifo chake ni pigo kubwa kwa jumuiya ya tasnini ya habari nchini humo. Ametuma salamu za rambirambi kwa familia, jamaa na marafiki wa Ali.

Magaidi wa Al Shabab

UNSOM imetoa wito kwa serikali ya Somalia kuhakikisha wahusika wa uhalifu huo wa kikatili wanafikishwa mbele ya mkono wa sheria.

Kundi la kigaidi la Al Shabab linashukiwa kutekeleza mauaji hayo kwani huko nyuma limewahi kuhusika na mauaji ya waandishi habari.