Burundi yasema haitawakamata baadhi ya wapinzani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1633-burundi_yasema_haitawakamata_baadhi_ya_wapinzani
Idara ya Mkuu wa Mashtaka wa Burundi imetangaza kuwa imefuta waranti wa kutiwa nguvuni idadi kadhaa ya watu wanaofuatiliwa kisheria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 20, 2016 23:18 UTC
  • Burundi yasema haitawakamata baadhi ya wapinzani

Idara ya Mkuu wa Mashtaka wa Burundi imetangaza kuwa imefuta waranti wa kutiwa nguvuni idadi kadhaa ya watu wanaofuatiliwa kisheria.

Kwa mujibu wa Idara hiyo, Mkuu wa Mashtaka wa nchi hiyo amefuta waranti wa kuwatia nguvuni watu 15 kati ya 34 wanaofuatiliwa kisheria wakiwemo viongozi kadhaa wa upinzani.

Katika hali ambayo mazungumzo kati ya serikali ya Rais Pierre Nkurunziza na wapinzani yamesita, uamuzi wa kufuta waranti wa kuwatia nguvuni watu hao 15 unaweza kuandaa mazingira ya kuanza tena mazungumzo hayo yenye lengo la kuutafutia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro ulioikumba nchi hiyo.

Miongoni mwa wanasiasa wa upinzani wanaoandamwa na serikali ya Bujumbura ni pamoja na Léonard Nyangoma, kiongozi wa chama cha CNARED, msemaji wa chama hicho Pancrace Cimpaye, Spika wa Bunge Pie Ntavyohanyuma na Makamu wa Pili wa Rais wa nchi hiyo Gervais Rufyikiri.

Burundi inashuhudia mgogoro mbaya zaidi tangu vilipomalizika vita vya ndani vilivyochochewa na ukabila mwaka 2005. Mgogoro huo uliosababishwa na Rais Pierre Nkurunziza kuwania tena urais kwa muhula wa tatu umesababisha mamia ya watu kuuawa na mamia ya maelfu kuihama nchi na kuwa wakimbizi katika nchi jirani.../