Wanachama 9 wa Boko Haram wauawa na jeshi la Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16390-wanachama_9_wa_boko_haram_wauawa_na_jeshi_la_nigeria
Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa, limewauwa wanachama 9 wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika mapigano yaliyojiri kati ya pande mbili kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 30, 2016 09:49 UTC
  • Wanachama 9 wa  Boko Haram wauawa na jeshi la Nigeria

Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa, limewauwa wanachama 9 wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika mapigano yaliyojiri kati ya pande mbili kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Sani Usman msemaji wa jeshi la Nigeria ameziambia duru za habari kwamba, wanajeshi wa nchi hiyo wamefanya mashambulio makubwa dhidi ya wanamgambo wa Boko Haram katika jimbo la Borno lililoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na kuwauwa wanachama 9 wa kundi hilo la kigaidi.

Msemaji wa jeshi la Nigeria ameongeza kuwa, wananchama wengi wa kundi hilo walijeruhiwa katika ubadilishanaji risasi kati ya pande mbili.

Aidha afisa huyo wa ngazi za juu wa jeshi la Nigeria amesema kuwa, jeshi lao limeazimia kuendelea na operesheni dhidi ya magaidi wa Boko Haram katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na kuyasafisha kabisa maeneo hayo na uwepo wa wanamgambo hao ambao wamekuwa wakifanya mauaji makubwa. Maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria yanahesabiwa kuwa ngome kuu ya kundi la kigaidi la Boko Haram. 

Wanachama wa Boko Haram

Wiki iliyopita pia wanamgambo 22 wa Boko Haram waliuawa na vikosi ya serikali katika operesheni ya jeshi la Nigeria dhidi ya ngome za wanamgambo hao.

Watu wasiopungua 20 elfu wameripotiwa kuuawa na wengine milioni mbili na laki sita wamepoteza makazi yao tangu kundi hilo la kitakfiri lilipoanzisha mashambulizi yake nchini Nigeria mwaka 2009.

Katika miaka ya hivi karibuni kundi hilo limepanua mashambulizi yake hadi katika nchi jirani za Cameroon, Niger na Chad.

Hivi sasa kumeundwa jeshi la nchi nne za Nigeria, Niger, Chad na Cameroon kwa ajili ya kupambana na genge hilo hasa kwenye eneo la Ziwa Chad.