Magaidi wa al-Qaidah 31 waliohusika na shambulizi Tunisia, wahukumiwa kifo
Mahakama nchini Tunisia imetoa hukumu ya adhabu ya kifo kwa magaidi 31 ambao walihusika katika shambulizi la kigaidi dhidi ya makazi ya Waziri wa Mambo ya Ndani mwaka 2014 nchini humo.
Sufyan al-Saliyati, afisa wa mahakama nchini Tunisia amenukuliwa akisema kuwa, mahakama ya nchi hiyo imewahukumu kifo wanachama hao wa genge la kigaidi la al-Qaidah kwa kushambulia makazi ya Lotfi Ben Jeddou, Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo. Amesema kuwa, katika shambulizi hilo lililotokea mwezi Mei mwaka 2014 katika mji wa Kasserine, kwa akali polisi wanne waliuawa na kwamba watu 46 walikuwa wakifuatiliwa katika faili la kesi hiyo.
Kadhalika mahakama ya Tunisia imewahukumu kifungo cha miaka mitatu hadi minane jela magaidi wanane katika kesi hiyo kwa kosa la kuwa wanachama wa genge la kigaidi huku watu saba wengine wakifutiwa mashitaka. Itakumbukwa kuwa, hukumu ya adhabu ya kifo ilisitishwa nchini Tunisia tangu mwaka 1991.
Ikumbukwe kuwa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Qaidah lilitangaza kuhusika na hujuma hiyo dhidi ya makazi ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tunisia.