Misri yaanza kusikiliza kesi kuhusu visiwa vya Sanafir na Tiran
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17050-misri_yaanza_kusikiliza_kesi_kuhusu_visiwa_vya_sanafir_na_tiran
Mahakama moja nchini Misri imeanza kusikiliza rufaa ya serikali ya Cairo ya kupinga uamuzi wa mahakama ya chini ya nchi hiyo wa kutaka Saudi Arabia ipokonywe visiwa vya kistratajia vya Tifan na Sanafir, milki ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 09, 2016 04:24 UTC
  • Misri yaanza kusikiliza kesi kuhusu visiwa vya Sanafir na Tiran

Mahakama moja nchini Misri imeanza kusikiliza rufaa ya serikali ya Cairo ya kupinga uamuzi wa mahakama ya chini ya nchi hiyo wa kutaka Saudi Arabia ipokonywe visiwa vya kistratajia vya Tifan na Sanafir, milki ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Khaled Ali, ambaye wakati mmoja aligombea urais nchini Misri na wakili mashuhuri wa haki za binadamu nchini humo amewasilisha ushahidi unaothibitisha kuwa visiwa hivyo viwili vinamilikiwa na Misri. Mwanaharakati huyo wa upinzani amewasilisha mahakamani hapo vielelezo vya nyaraka zikiwemo ramani za jadi za hadi karne ya 20, zinazoonyesha kuwa visiwa hivyo vipo ndani ya Misri.

Hata hivyo mawakili wa serikali wameiambia mahakama hiyo kuwa Saudia ililazimika kuukabidhi utawala wa Misri visiwa hivyo kwa muda mwaka 1950, ikihofia kushabuliwa na utawala haramu wa Israel.

Rais Abdul Fatah al-Sisi wa Misri na Mfalme Salman wa Saudia

Itakumbukwa kuwa, mwezi Aprili mwaka huu, Taqadum Al-khatib, mwanaharakati mwingine mashuhuri ambaye pia ni mtafiti raia wa Misri anayeishi Ujerumani, aliliambia gazeti la As-Safir linalochapishwa mjini Bairut nchini Lebanon kuwa, ramani iliyoko katika maktaba ya mjini Berlin, Ujerumani na kadhalika ramani zote za dunia, zinathibitisha wazi kwamba, visiwa hivyo viwili vya Sanafir na Tiran vilivyoko katika Ghuba ya Aqaba ni mali ya Misri na sio Saudia.

Hatua ya Rais Abdul Fattah al-Sisi wa Misri ya kumpatia Mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudia visiwa vya Sanafir na Tiran na kudai kuwa, michoro ya kimipaka baharini inaonyesha kwamba, visiwa hivyo vilivyoko Bahari Nyekundu viko katika maji ya Saudia, ilipokewa kwa hasira na wananchi wa Misri walioingia barabarani na kufanya maandamano kwa siku kadhaa.