Wananchi Niger walalamikia uendeshaji mbovu wa uchaguzi
Wananchi wa Niger wameilalamikia vikali serikali ya nchi hiyo kwa kuendesha vibaya uchaguzi.
Vyombo vya habari vimewanukuu wananchi hao wakilalamikia uendeshaji mbovu wa uchaguzi wa Rais uliofanyika jana nchini humo na kusema kuwa tume ya uchaguzi ya nchi hiyo imevuruga kwa makusudi uchaguzi huo kwa maslahi ya rais aliyeko madarakani.
Mashirika hayo yamewanukuu wananchi wakilalamika kuwa, tume ya uchaguzi imeweka vizuizi vingi vilivyopelekea watu wengi washindwe kutumia haki yao ya kupiga kura hiyo jana.
Vituo vingi vya kupigia kura vilifunguliwa kwa kuchelewa, huku baadhi ya vituo hivyo vikishindwa kupiga kura kabisa kutokana na kuchelewa vifaa vya kupigia kura kama vile karatasi na masanduku ya kura.
Rais Mahamadou Issoufou amegombea kwa mara ya pili katika uchaguzi huo.
Katika upande mwingine wapinzani wanasema kuwa, udanganyifu mkubwa uliofanyika kwenye uchaguzi huo wa jana umemuandalia ushindi Mahamadou Issoufou.