Wapinzani wakusanyika Kisangani wakitaka kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa
Wapinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamekusanyika katika mji wa Kisangani nchini humo wakitaka kuachiwa huru wanaharakati wa kisiasa wanaoipinga serikali.
Benjamin Ntumba mmoja wa wanaharakati wa chama cha Upinzani cha Umoja kwa ajili ya Demokrasia na Maendeleo ya Jamii (UDPS) amesema kuwa wapinzani Kongo wamekusanyika katika mji wa Kisangani kulalamikia hatua ya Mahakama moja mjini humo ya kukataa kuwaachia huru wapinzani sita wa kisiasa.
Wanaharakati hao sita wa kisiasa wanaoipinga serikali ya Kinshasa wanashikiliwa mahabusu huko Kisangani tangu tarehe 19 mwezi uliopita hadi sasa. Benjamin Ntumba ameashiria kuachiwa huru watu wengine ambao walitiwa mbaroni pamoja na wanaharakati hao sita na kusisitiza kuwa, wanaharakati hao wa kisiasa wanaoipinga serikali ya Kongo wamekatwa kinyume cha sheria. Ntumba ametaka wanaharakati hao waachiwe huru haraka na bila ya masharti yoyote.