Machafuko Burundi, kiongozi wa chama tawala auawa na watu wasiojulikana
Mmoja wa viongozi wa chama tawala CNDD-FDD nchini Burundi ameripotiwa kuuawa katika shambulizi lililofanywa na watu wasiojulikana.
Joachim Manirakiza, afisa wa mkoa wa Rumonge nchini Burundi amenukuliwa na vyombo vya habari leo akisema kuwa, watu watatu akiwemo kiongozi wa ngazi ya juu katika chama tawala nchi humo, wameuawa na watu wasiojulikana kwenye baa moja katika kijiji cha Saga kilichopo mkoani hapo.
Kufuatia shambulizi hilo, chama tawala kimeitaja hujuma hiyo kuwa ni katika mwendelezo wa matukio ya ukatili wa kisiasa yanayoendelea nchini. Hadi sasa washambuliaji bado hawajajulikana.
Machafuko ya ndani nchini Burundi yaliibuka mwezi April mwaka jana baada ya chama tawala CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kugombea muhula wa tatu katika uchaguzi wa rais uliopita. Katika machafuko hayo mamia ya watu wameuawa na maelfu ya wengine kuwa wakimbizi.
Kufuatia hali hiyo wiki iliyopita, Umoja wa Mataifa ulikubali pendekezo la kuanzishwa tume maalumu ya uchunguzi kwa lengo la kuwabaini wahusika wa mauaji na ukiukwaji wa haki za binaadamu ndani ya taifa hilo.