Kupigwa marufuku shughuli za harakati ya Kiislamu ya Nigeria
Viongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) wamelaani uamuzi uliopitishwa na Gavana wa jimbo la Kaduna Nasir Ahmed el-Rufai wa kupiga marufuku shughuli za harakati hiyo.
Uamuzi huo umepitishwa baada ya Waislamu katika jimbo hilo ambao ni wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria kuandamana katika eneo la Funtawa kutaka kiongozi wa harakati hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky aachiliwe huru. Sheikh Zakzaky alitiwa nguvuni mwezi Desemba mwaka jana kwa tuhuma za kuchochea wananchi kuandamana dhidi ya serikali na hivi sasa yuko kwenye kizuizi cha nyumbani.
Wakati huohuo watu wasiopungua 20 waliuawa katika machafuko yaliyotokea baada ya vikosi vya usalama vay serikali ya Nigeria kuvamia hafla ya maombolezo ya Ashura katika jimbo la Kaduna, kaskazini mwa nchi hiyo. Waislamu duniani kote huwa kila mwaka wanafanya maombolezo kwa mnasaba wa Tasua na Ashura (siku za mwezi 9 na 10 Muharram). Hata hivyo Waislamu wa Kaduna waliojitokeza mabarabarani kuadhimisha kumbukumbu hiyo ya mapambano ya Imam Hussein (as) dhidi ya kufuru na dhulma walikabiliwa na ukandamizaji wa mkono wa chuma wa vikosi vya usalama. Kabla ya hapo pia askari wa jeshi la Nigeria waliuzingira msikiti wa Waislamu hao katika jimbo hilo la Kaduna. Hatua hiyo iliamsha moto wa hasira za Waislamu ambao walijitokeza kuandamana kutaka kuondolewa mzingiro huo na kuachiwa huru wenzao 15 waliokuwa wametiwa nguvuni na polisi.
Kwa mtazamo wa wadadisi wa mambo, muamala wa viongozi wa jimbo la Kaduna dhidi ya Waislamu unatekelezwa kukidhi sera za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel. Kuendelea kushamiri na kupata nguvu dini tukufu ya Uislamu katika eneo la kaskazni mwa Nigeria na vile vile kuzidi kupata umashuhuri na kuongezeka mapenzi ya watu kwa kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky kumeukanganya na kuutia kiwewe utawala wa Kizayuni. Kutiwa hofu utawala haramu wa Israel na ongezeko la idadi ya Waislamu nchini Nigeria ambayo kutokana na kuwa na idadi ya watu wapatao milioni 180 ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika kuna uhusiano wa moja kwa moja na ukandamizaji wa umwagaji uliofanywa dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo katika maombolezo ya Muharram.
Katika hali ambayo maombolezo ya Muharram ya Waislamu katika jimbo la Kaduna hayasababishi madhara yoyote kwa serikali ya Jimbo la Kaduna wala serikali kuu ya Nigeria, wadadisi wa mambo wanaitakidi kuwa wasiwasi na hofu ya kupata nguvu fikra na itikadi za Kiislamu ndiyo sababu iliyovifanya vikosi vya usalama vivamie mkusanyiko wa amani wa Waislamu hao.
Vitendo hivyo vya ukatili na utumiaji mabavu vinaweza kutathminiwa katika muelekeo wa utekelezaji mpango wa "Kueneza hofu na chuki dhidi ya Uislamu" kwa kimombo Islamophobia ambao baada ya matukio ya Septemba 11, 2001 ulianza kutumiwa kama kisingizio cha kuwanyanyasa na kuwabughudhi Waislamu duniani. Viongozi wa baadhi ya nchi za Magharibi ikiwemo Marekani wanatumia kila mbinu kulihusisha tukio la Septemba 11 na Uislamu ili kupenyeza ndani ya fikra za walimwengu hisia za hofu na chuki dhidi ya dini ya Kiislamu na kufanikisha mpango wa huo wa kueneza hofu na chuki juu ya dini hiyo tukufu. Mpango ambao bila ya shaka yoyote umeandaliwa kwa mikakati maalumu ili kuwafaidisha wapangaji wake wenye malengo ya kidhalimu na kibeberu.
Kuchochea hitilafu na mifarakano baina ya Waislamu kwa kisingizio cha kutafautiana kwao katika ufahamu wao juu ya dini yao, na kwa sababu ya mitazamo tofauti iliyopo baina yao juu ya masuala mbalimbali ya kiimani na kimadhehebu ni wenzo ambao serikali ya jimbo la Kaduna imeutumia katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kwa maslahi yake. Lakini mbali na hayo msimamo ulioonyeshwa na serikali kuu ya Nigeria wa kutojali wala kushughulishwa na mwenendo wa kikatili na kinyama wa vikosi vya usalama katika jimbo la Kaduna dihidi ya Waislamu ni wa kutafakari na wa kuzingatiwa mno, japokuwa mienendo hiyo ya kionevu ya serikali ya Abuja imekuwa ikishuhudiwa tangu mwezi Desemba mwaka uliopita wa 2015 wakati askari wa jeshi la Nigeria walipovamia mkusanyiko wa Waislamu katika mji wa Zaria, wakaua na kujeruhi maelfu ya watu na kumtia nguvuni pia Sheikh Ibrahim Zakzaky. Kugunduliwa maiti zipatazo 347 za wafuasi wa harakati ya Kiislamu ya Nigeria katika mji huo kumezidi kuwadhihirishia walimwengu ukubwa wa jinai za kutisha zilizofanywa na vikosi vya usalama vya Nigeria katika jimbo la Kaduna.../