Wapinzani Kongo watakiwa kujongea kwenye meza ya mazungumzo ya kitaifa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17467-wapinzani_kongo_watakiwa_kujongea_kwenye_meza_ya_mazungumzo_ya_kitaifa
Jumuiya ya Ustawi ya Kusini mwa Afrika (SADC) imewatolea wito wapinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kujiunga na mazungumzo ya kitaifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 15, 2016 09:12 UTC
  • Wapinzani Kongo watakiwa kujongea kwenye meza ya mazungumzo ya kitaifa

Jumuiya ya Ustawi ya Kusini mwa Afrika (SADC) imewatolea wito wapinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kujiunga na mazungumzo ya kitaifa.

Idara ya Ushirikiano wa Kisiasa, Kiulinzi na Kiusalama ya Jumuiya ya SADC imetoa taarifa ikiwataka wapinzani nchini Kongo DR kushiriki kwenye mazungumzo ya kitaifa ili kufikia mapatano. Ujumbe wa SADC umeashiria mafanikio yaliyopatikana katika mazungumzo ya kitaifa ya Kongo na mchakato wa kuwaandikisha wapiga kura unaofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo (CENI) na kuwataka viongozi wote wa kisiasa wa Kongo kuandaa mazingira mazuri ya kufanikisha uchaguzi ulio huru, wa kiadilifu, wa wazi na wenye itibari.

Ujumbe huo wa SADC unaoongozwa na Augustine Mahiga Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania umeelekea Kongo DR  kutathmini hali ya kisiasa na kiusalama ya nchi hiyo na juhudi zinazotekelezwa kwa lengo la kudumisha amani na uthabiti wa kisiasa huko Kongo.

Dr Augustine Mahiga Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania ambaye anaongoza ujumbe wa SADC huko Kongo

Mivutano ya kisiasa imeongezeka huko Kongo kufuatia kutangazwa rasmi kuakhirishwa tarehe ya uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo hadi mwaka 2018. Wapinzani wanaamini kuwa kitendo cha kuakhirisha uchaguzi huo ni kisingizio tu kinachotumiwa na Rais Kabila ili aweze kusalia madarakani. Wapinzani hao wanasema kuwa kuakhirishwa uchaguzi wa Rais wa Kongo kutaandaa njia ya kufanyika udanganyifu au kutekelezwa mabadiliko ya kisheria yatakayomuwezesha kuendelea kubaki madarakani Rais Joseph Kabila. Hata hivyo maafisa husika wa Kongo wanasema kuwa tarehe ya kufanyika uchaguzi wa Rais imeahirishwa lengo likiwa ni kuandaa mazingira yanayohitajika na kuvutia ushiriki mkubwa wa wapiga kura kwenye uchaguzi huo. Siku kadhaa zilizopita Rais Joseph Kabila aliwajibu wapinzani kwa kusema kuwa, wananchi wa Kongo zaidi ya milioni kumi watapoteza fursa ya kupiga kura iwapo uchaguzi hautaakhirishwa.

Rais Joseph Kabila anayekabiliwa na mashinikizo makubwa ya wapinzani  ili ang'atuke madarakani

Hatua za serikali ya Kabila khususan katika wiki kadhaa zilizopita zimeibua mivutano ya kisiasa ambayo ilisababisha maandamano ya mitaani  na kushadidisha machafuko nchini humo. Aidha siku kadhaa zilizopita maandamano ya wapinzani dhidi ya serikali yalisabisha mapigano makali ya umwagaji damu  kati ya wafanya maandamano na polisi, na kupelekea pia kuchomwa moto majengo ya serikali katika mitaa ya mji mkuu Kinshasa na kushadidisha pia hali ya mchafukoge katika miji ya nchi hiyo. Wimbi la machafuko hayo lilijiri tarehe19 na 20 mwezi Septemba mwaka huu na kusababisha vifo vya waandamanaji kadhaa na wengine wengi kujeruhiwa.

Weledi wengi wa mambo wanaamini kuwa wito uliotolewa na Jumuiya ya SADC kwa wapinzani wa Kongo ili kushiriki mazungumzo ya kitaifa ni juhudi nyingine zenye lengo la kuzuia kushtadi na kuendelea machafuko nchini humo.