Waliouawa katika mapigano ya kikabila nchini Nigeria wafikia 40
Duru za hospitali nchini Nigeria zimeripoti ongezeko la watu waliouawa katika mapigano ya kikabila kaskazini mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa duru hizo, mapigano hayo ya wakulima kutoka kabila la Fulani yamejiri katika eneo la Godogodo lililopo katika jimbo la Kaduna, kaskazini mwa Nigeria ambapo kwa akali watu 40 wameuawa. Habari zaidi zinaarifu kuwa, kushadidi machafuko hayo ya kikabila katika eneo hilo la kiuchumi, kumeifanya serikali ya Nigeria kuchukua hatua ya kutuma askari kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro huo uliopewa jina la 'Uasi wa Fulani' katika jimbo la Kaduna.
Hii ni katika hali ambayo hujuma za wakulima kutoka kabila la Fulani katika maeneo tofauti ya jimbo hilo, zimeibua hali ya wasi wasi mkubwa baina ya wakazi wa maeneo hayo. Akthari ya watu wa kabila la Fulani wanaishi katika maeneo tofauti ya Nigeria, huku wengi wao wakijishughulisha na uvuvi na kilimo.
Kwa miaka kadhaa sasa eneo la Godogodo limekuwa likishuhudia wimbi la mapigano na ukatili wa kikabila na kupelekea mamia ya watu kuuawa. Migogoro ya kikabila na kikaumu ni changamoto nyingine inayolikabili taifa la Nigeria baada ya hujuma za wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram na mashambulio ya waasi wa eneo la Niger Delta.