Harakati ya Kiislamu Nigeria kotini kupinga marufuku dhidi yake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17881-harakati_ya_kiislamu_nigeria_kotini_kupinga_marufuku_dhidi_yake
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imeelekea mahakamani kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa serikali kupiga marufuku shughuli za harakati hiyo katika jimbo la Kaduna.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Oct 21, 2016 10:31 UTC
  • Harakati ya Kiislamu Nigeria kotini kupinga marufuku dhidi yake

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imeelekea mahakamani kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa serikali kupiga marufuku shughuli za harakati hiyo katika jimbo la Kaduna.

Taarifa ya harakati hiyo imesema kuwa, uamuzi huo wa viongozi wa jimbo la Kaduna unakinzana na katiba ya nchi, ambayo imemdhaminia kila mmoja haki na uhuru wa kuabudu.

Hivi karibuni harakati hiyo ya Kiislamu ilipigwa marufuku katika jimbo la Kaduna, hatua ambayo imelalamikiwa vikali na watetezi wa haki za binadamu na makundi ya kiraia.

Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria ambaye yuko kizuizini tangu Disemba 2015

Gavana wa jimbo la Kaduna, Nasir Ahmed el-Rufai alionya kuwa, yeyote atakayepatikana kuwa mwanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria atafungwa jela miaka saba au kutozwa faini au yote mawili kwa pamoja. Aidha serikali ya Kaduna ilidai kuwa, Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambayo aghalabu ya wanachama wake ni Waislamu wa madhehebu ya Shia imekuwa ikishiriki katika maandamano yasiyo na kibali na kuzuia magari barabarani tangu Disemba mwaka jana.

Marufuku hiyo ilipitishwa baada ya wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria katika jimbo hilo kuandamana katika eneo la Funtawa kutaka kiongozi wa harakati hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky aachiliwe huru.

Ukatili wa jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu

Mienendo hiyo ya kionevu ya serikali ya Abuja dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia imekuwa ikishuhudiwa tangu mwezi Disemba mwaka uliopita wa 2015, wakati askari wa jeshi la nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika walipovamia mkusanyiko wa Waislamu katika mji wa Zaria, wakaua na kujeruhi maelfu ya watu mbali na kumtia nguvuni Sheikh Ibrahim Zakzaky.