Serikali ya Burundi yakubali pendekezo la kuzungumza na wapinzani
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema kuwa serikali ya Burundi imekubaliana na pendekezo la kufanya mazungumzo na wapinzani. Ban Ki-moon ameyasema hayo leo huko Bujumbura, mji mkuu wa Burundi na kuongeza kuwa, serikali ya nchi hiyo imeahidi pia kuanzisha mazungumzo ya kina na ya pamoja na wapinzani wake.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ameyasema hayo baada ya mazungumzo yake na Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi na kufafanua kuwa, rais huyo ameafiki pia kufanya juhudi kwa ajili ya kufanikisha mazungumzo hayo ya kisiasa nchini humo. Akiashiria mazungumzo ya jana usiku na viongozi wa vyama vya upinzani nchini Burundi, Ban Ki-moon amesema kuwa, kuanzia sasa hakutakuwa na kikwazo chochote kitakachozuia kuitisha na kuendelezwa mazungumzo hayo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliwasili jana jioni mjini Bujumbura kwa lengo la kuzishawishi pande husika nchini humo kurejea kwenye meza ya mazungumzo, baada ya serikali ya Bujumbura kususia mazungumzo hayo kwa muda sasa. Katika fremu hiyo Rais Nkurunziza alikuwa ametangaza kuwa, serikali yake iko tayari kufanya mazungumzo na Warundi wote isipokuwa tu wale alioawaita kuwa magaidi ambao wanaendesha machafuko nchini humo ili kumuondoa madarakani. Mgogoro wa Burundi uliibuka mwezi Aprili mwaka jana, baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza azma yake ya kugombea kwa mara ya tatu uchaguzi uliopita.