Waasi wa Niger Delta: Tumeshambulia bomba la mafuta la kampuni ya Chevron
Kundi la wanamgambo wanaojiita Walipizaji Kisasi wa Niger Delta limetangaza kuwa limeshambulia bomba la mafuta katika eneo la uzalishaji nishati hiyo kusini mwa Nigeria na kuyaonya makampuni ya kigeni ya mafuta kutoyafanyia matengenezo mabomba hayo yaliyoharibiwa.
Kundi hilo ambalo lilikuwa limetangaza kuacha uhasama wake na serikali ya Nigeria ili kufanya mazungumzo na serikali limetangaza kupitia tovuti yake kuwa limeshambulia na kuharibu bomba la kusafirishia mafuta la kampuni ya kimataifa ya Chevron katika fukwe za eneo la Escravos alfajiri ya kuamkia leo.
Collins Edema, kiongozi wa eneo la Niger Delta amesema wamepata taarifa za tukio hilo katika pwani za eneo la Escravos lakini hakuna ajuae ukubwa wa maafa yaliyosababishwa na uripuaji huo.
Kundi la Walipizaji Kisasi wa Niger Delta limesisitiza kuwa linataka fungu kubwa zaidi la pato la fedha zinazotokana na uuzaji mafuta lipelekwe eneo la Niger Delta ambalo ndilo linalozalisha kiwango kikubwa zaidi cha mafuta ghafi ya Nigeria.
Duru za serikali zimeviarifu vyombo vya habari kuwa serikali ya Abuja itakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa jamii ya eneo la Niger Delta na wawakilishi wa kundi hilo la wanamgambo wiki ijayo.../