Misri yaidhinisha kifungo cha maisha jela dhidi ya kiongozi wa Ikhwani
Mahakama ya Rufaa nchini Misri jana Jumatano ilitilia nguvu hukumu iliyotolewa na mahakama ya chini ya kifungo cha maisha jela kwa kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin.
Mahakama hiyo imesema Mohamed Badie na wenzake 36 ambao walihudumu kama mawaziri kati ya mwaka 2011 na 2013, wanastahili kufungwa jela maisha kwa tuhuma za kuchochea machafuko na mauaji nchini humo. Aidha mahakama hiyo imeidhinisha uamuzi wa kuwanyonga wafuasi 10 wa Ikhwan, licha ya kwamba hawakuweko mahakamani wakati wa kutolewa hukumu hiyo.
Awali mahakama ya jinai ya Misri ilikuwa imemhukumu kifo kiongozi huyo wa Ikhwan. Hata hivyo, kamisheni ya haki za binadamu nchini humo na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za kibinadamu yalishinikiza kufutwa hukumu hiyo dhidi ya viongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin akiwemo Mohammed Badie.
Badie ambaye alikuwa na nafasi kubwa katika kuanzisha vuguvugu lililomng'oa madarakani dikteta wa zamani wa nchi hiyo Hosni Mubarak, alihukumiwa adhabu ya kifo na mahakama moja ya nchi hiyo akiwa pamoja na wanachama wengine 682 wa Ikhwanul Muslimin, mwaka 2014.
Mahakama moja ya Misri tarehe 11 mwezi Aprili mwaka jana iliidhinisha kunyongwa Muhammad Badie na maafisa wengine 13 wa kundi hilo mbali na kuwahukumu kifungo cha maisha jela maafisa wengine 36 wa Ikhwan.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Jumamosi iliyopita, Mahakama ya Rufaa nchini Misri ilipasisha rasmi hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela dhidi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Muhammad Morsi kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya wapinzani katika maandamano ya mwaka 2012.