Wapinzani Mauritania wataka kufanya mazungumzo na serikali
Baadhi ya wapinzani nchini Mauritania wametaka kufanya mazungumzo mapya na serikali.
Katika hali ambayo baadhi ya wapinzani huko Mauritania wametaka kufanya mazungumzo mapya na wawakilishi wa serikali, chama tawala cha Umoja kwa ajili ya Jamhuri kimesisitiza kufanyika kura ya maoni kuhusu kuifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo.
Kufutwa bunge la Seneti na kuundwa serikali za mitaa yanatajwa kuwa moja ya marekebisho muhimu yanayopaswa kutekelezwa katika katiba ya nchi hiyo. Rais Mohammed Ould Abdulaziz wa Mauritania amesisitiza kuwa atajiuzulu uongozi baada ya kumalizika duru yake ya pili ya urais mwaka 2019 kama ilivyoainishwa na katiba; jambo ambalo limeungwa mkono kwa tahadhari na wapinzani nchini humo. Wakati huo huo wapinzani wamewatolea wito wananchi kufanya maandamano kupinga marekebisho hayo ya katiba.