Nigeria yaanzisha miradi ya miundo msingi kuzuia uasi Niger Delta
Serikali ya Nigeria imezindua miradi ya miundo msingi itakayogharimu dola bilioni 10 katika eneo linalokumbwa na uasi la Niger Delta ili kumaliza uasi huo.
Waziri wa Mafuta wa Nigeria Emmanuel Ibe Kachikwu alizindua mradi huo Alhamisi na kusema Rais Muhammadu Buhari atakutana na wawakilishi wa makundi ya waasi na viongozi wa kijamii wiki ijayo ili kujadili njia za kusitisha mashambulizi dhidi ya taasisi za mafuta eneo hilo.
Amesema kitita hicho cha dola bilioni 10 kitatolewa na serikali pamoja na wawekezaji, mashirika ya mafuta na watu binafsi katika eneo hilo.
Katika miezi ya hivi karibuni Kundi la waasi wanaojiita Walipizaji Kisasi wa Niger Delta wamekuwa wakishambulia mabomba ya mafuta katika eneo la uzalishaji nishati hiyo kusini mwa Nigeria na kuyaonya makampuni ya kigeni ya mafuta kutoyafanyia matengenezo mabomba hayo yaliyoharibiwa.
Kundi la Walipizaji Kisasi wa Niger Delta limesisitiza kuwa linataka fungu kubwa zaidi la pato la fedha zinazotokana na uuzaji mafuta lipelekwe eneo la Niger Delta ambalo ndilo linalozalisha kiwango kikubwa zaidi cha mafuta ghafi ya Nigeria ambayo ni kati ya nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani.
Wakaazi wa eneo la Delta, ambao baadhi yao wanayaunga mkono makundi ya wanamgambo, wamekuwa kwa muda mrefu wakilalamikia hali ya umasikini ya eneo lao hilo ambalo linazalisha mafuta yanayodhamini asilimia 70 ya pato lote la taifa la Nigeria.
Wanamgambo wa eneo hilo la Niger Delta wanamtuhumu Rais Muhammadu Buhari kwa kutojali maslahi ya wananchi wa nchi hiyo.