Kodivaa washiriki kura ya maoni kuainisha katiba mpya
Wapiga kura nchini Kodivaa (Ivory Coast) leo wameshiriki katika kura ya maoni ya kuamua iwapo katiba mpya ya nchi hiyo iidhinishwe au la huku wapinzani wakitaka kususiwa kura hiyo.
Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast anasema katiba mpya iliyopendekezwa itadhamini amani katika nchi hiyo iliyoathiriwa na mchafuko ya kisiasa kwa miaka kadhaa.
Wananchi wa Ivory Coast wameendelea kugawanyika kisiasa na kikabila licha ya nchi hiyo kushuhudia amani katika miaka kadhaa ya hivi karibuni. Rais Ouattara amesema kuwa katiba hiyo mpya iliyopendekezwa ni nzuri kwa kuwa italeta mabadiliko makubwa ya maana nchini humo.
Wapinzani nchini Ivory Coast wamesusia kushiriki katika kura hiyo ya maoni ya kuainisha katiba mpya wakisema kuwa, rasimu hiyo ya katiba imebuniwa ili kuuimarisha zaidi muungano wa kisiasa wa Rais Alassane Ouattara. Katiba ya hivi sasa ya Kodivaa ambayo iliandaliwa chini ya utawala wa kijeshi baada ya mapinduzi ya mwaka 1999, imekuwa ni sababu kuu ya machafuko ya muda mrefu katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.