Kuendelea mageuzi ya kisiasa nchini Ivory Coast
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18808-kuendelea_mageuzi_ya_kisiasa_nchini_ivory_coast
Kufuatia kufanyika Kura ya Maoni ya marekebisho ya Katiba ya Ivory Coast, serikali ya nchi hiyo imetangaza tarehe ya kufanyika uchaguzi wa Bunge la nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 04, 2016 16:05 UTC
  • Kuendelea mageuzi ya kisiasa nchini Ivory Coast

Kufuatia kufanyika Kura ya Maoni ya marekebisho ya Katiba ya Ivory Coast, serikali ya nchi hiyo imetangaza tarehe ya kufanyika uchaguzi wa Bunge la nchi hiyo.

Mara baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika jana, msemaji wa serikali ya Ivory Coast  Bruno Koné, alitangaza kuwa uchaguzi wa bunge utafanyika tarehe 18 ya mwezi ujao wa Desemba.

Tarehe hiyo imependekezwa na Tume Huru ya Uchaguzi ya nchi hiyo.

Koné ameeleza kuwa tarehe 18 Desemba Wakodivaa wataelekea vituo vya kupigia kura kuwachagua wabunge 225, ambao tab'an wengi wao wanatoka chama tawala nchini humo.

Tarehe ya uchaguzi wa bunge imetangazwa katika hali ambayo baada ya mivutano na misuguano mingi ya kisiasa kuhusu kura ya maoni ya marekebisho ya katiba, kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi  zaidi ya asilimia 90 ya wananchi walioshiriki kwenye kura hiyo ya maoni wameunga mkono marekebisho ya katiba yaliyopendekezwa na rais wa nchi hiyo Alassane Ouattara. Kwa mujibu wa tume hiyo asilimia 93.42 ya watu walioshiriki kwenye zoezi la kura ya maoni  iliyofanyika siku ya Jumapili ya tarehe 30 Oktoba walipigia kura ya "Ndiyo" mabadiliko ya katiba yaliyopendekezwa.

Rais Alassane Ouattara aliposhiriki katika kura ya maoni

Kufuatia kupitishwa mabadiliko hayo, kifungu cha katiba kinachoeleza kwamba mgombea urais lazima atokane na wazazi ambao ni wazaliwa wa Ivory Coast kitafutwa.

Kuondolewa kikomo cha umri wa miaka 75 kwa wagombea wa uchaguzi na kuanzishwa Baraza la Seneti ni vifungu vingine vitakavyokuwemo kwenye katiba mpya ya nchi hiyo.

Kutokana na Kura ya Maoni iliyofanyika Oktoba 30 ambayo matokeo yake yanapasa yaidhinishwe na Baraza la Katiba, katiba hiyo itakuwa ya tatu kupitishwa nchini Ivory Coast.

Katiba ya pili ilikuwa ni ile iliyopitishwa mwezi Agosti mwaka 2000, miezi sita baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1999, ambapo asilimia 87 ya Wakodivaa walioshiriki kwenye kura ya maoni waliunga mkono kufanyiwa mabadiliko katiba ya nchi yao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki moon amekaribisha kupitishwa katiba mpya ya Ivory Coast na kueleza kwamba katiba hiyo itaondoa baadhi ya sababu za muda mrefu zilizochochea kuzuka hitilafu na mivutano katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Katibu Mkuu wa UN Ban Ki moon

Aidha ametaka uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika wiki kadhaa zijazo ufanyike katika anga huru, ya haki na uwazi.

Katibu Mkuu wa UN amezihimiza pande zote nchini Ivory Coast hasa viongozi wa kisiasa na wafuasi wao kujiepusha na ghasia na machafuko na kutumia lugha za kueneza ftina na uchochezi.

Mabadiliko ya katiba ya Ivory Coast yameungwa mkono katika hali ambayo vyama vya upinzani vimefanya mikusanyiko mara kadhaa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kupinga na kulalamikia suala hilo. Vyama hivyo aidha vilisusia zoezi la kura ya maoni na kuwataka wafuasi wao wasishiriki bali hata wazuie kufanyika zoezi hilo.

Wawakilishi wa mrengo wa upinzani wanamtuhumu Rais Ouattara kwamba hatua yake ya kutaka kuanzisha cheo cha Makamu wa Rais na kuunda Baraza la Seneti kupitia mabadiliko ya katiba inalenga kuhodhi madaraka kwa manufaa ya vyama vinavyomuunga mkono.

Maandamano ya upinzani nchini Ivory Coast

Kwa mujibu wa wapinzani hao kuundwa Baraza la Seneti, mbali na kumpa kiongozi huyo mamlaka ya kuwachagua wajumbe 30 kati ya wajumbe wote 100, kutapunguza pia mamlaka ya bunge na kulibebesha taifa hilo gharama kubwa za matumizi ya fedha.

Aidha kwa kuanzisha cheo cha umakamu wa rais, endapo rais atafariki au kuachia hatamu za uongozi makamu wake ndiye atakayekalia kiti cha urais hadi mwisho wa kipindi cha uongozi wake.

Wapinzani wao wanasema kipengee hicho kinaweza kumfungulia njia rais ya kuandaa na kuteua mrithi wake.

Japokuwa wafuatiliaji wa siasa za Ivory Coast wangali na wasiwasi juu ya hali ya kisiasa ya nchi hiyo na hata baadhi yao kutabiri kuwa mnamo siku chache zijazo wapinzani wataonesha misuli yao kwa kupinga matokeo ya kura ya maoni, lakini kwa mtazamo wao, matokeo ya kura hiyo ya maoni yameonesha kuwa baada ya miaka ya vita na mivutano Wakodivaa sasa wanataka nidhamu na uthabiti wa kisiasa urejee nchini mwao.

Kabla ya hapo Rais Alasane Ouattara alikuwa amesisitizia ulazima wa kuwepo mshikamano wa kisiasa nchini baada ya zoezi la kura ya maoni. Matarajio yaliyopo ni kumwona yeye mwenyewe akitekeleza kivitendo ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi ikiwemo kuboresha hali ya uchumi na kuhakikisha amani na usalama unatawala nchini humo.../