UN: Al Shabab ingali tishio kubwa kwa Somalia, Afrika Mashariki
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18829-un_al_shabab_ingali_tishio_kubwa_kwa_somalia_afrika_mashariki
Magaidi wakufurishaji wa kundi la Al Shabab wametajwa kuwa tishio kubwa sana kwa nchi ya Somalia na eneo zima la mashariki mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 05, 2016 01:04 UTC
  • UN: Al Shabab ingali tishio kubwa kwa Somalia, Afrika Mashariki

Magaidi wakufurishaji wa kundi la Al Shabab wametajwa kuwa tishio kubwa sana kwa nchi ya Somalia na eneo zima la mashariki mwa Afrika.

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imeonya kuwa, magaidi wa Al Shabab walioko Somalia bado wana uwezo wa kutekeleza mashambulizi makubwa pamoja na kuwepo taarifa za mafanikio katika jitihada za kupambana na ugaidi nchini humo.

Kundi la Al Shabab, linalofungamana na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda, limetekeleza hujuma kubwa dhidi ya hoteli kadhaa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu kati ya Novemba 2015 na Juni 2016. Ripoti hiyo iliyochapishwa na wakaguzi wa Umoja wa Mataifa Ijumaa imesema, kundi hilo la magaidi wakufurishaji, ‘ni hatari kwa usalama na uthabiti Somalia na pia linaendelea kuvuruga uthabiti katika eneo zima la Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika.”

Ripoti hiyo ambayo imekabidhiwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imeashiria hujuma ya mwaka 2015 dhidi ya Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya ambayo watu zaidi ya 150 waliuawa na kusema, “Al Shabab ingali ina uwezo wa kutekeleza shambulizi kama hilo kwani imetangaza azma ya kuzilenga nchi ambazo zimetuma askari katika Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika Somalia, AMISOM.”

Nchi ambazo zina askari katika kikosi cha AMISOM ni pamoja na Kenya, Ethiopia, Uganda, Burundi, Djibouti na Sierra Leone. Miongoni mwa nchi hizo, Kenya ndiyo ambayo imekuwa ikilengwa zaidi na Al Shabab. Ripoti hiyo pia imeikosoa serikali ya Somalia kwa kushindwa kuwalipa askari mishahara yao jambo ambalo limepelekea magaidi wa Al Shabab kurejea katika eneo la kusini na kati mwa nchi hiyo.